Lugha Nyingine
Msimu wa uuzaji tumbaku nchini Zimbabwe kwa Mwaka 2024 wafunguliwa
Askari Polisi wa Zimbabwe wakiwa katika kazi ya ulinzi kwenye hafla ya ufunguzi wa msimu wa uuzaji tumbaku kwa Mwaka 2024 huko Harare, Zimbabwe, Machi 13, 2024. (Picha na Shaun Jusa/Xinhua)
HARARE - Msimu wa uuzaji tumbaku kwa Mwaka 2024 nchini Zimbabwe umefunguliwa Jumatano, huku kukiongezeka kwa wito wa uzalishaji wa tumbaku inayohimili mabadiliko ya tabianchi wakati kukiwa na hali ya mvua isiyotabirika ambapo Makamu Rais wa Zimbabwe Constantino Chiwenga amesema wakati uzalishaji wa tumbaku nchini humo unakadiriwa kuwa chini kidogo mwaka huu kuliko kilo milioni 296 za tumbaku zilizorekodiwa msimu uliopita, lakini msimu wa uuzaji unatarajiwa.
"Hatuwezi kupata kilo milioni 300 tulizotaka, lakini nina furaha kwamba mazao yaliyopatikana kwa umwagiliaji yameonekana kuwa mazuri, na ni mazao ya nchi kavu ambayo yameathirika kidogo, lakini msimu unaonekana mzuri 2024," Chiwenga amesema katika hotuba yake ya ufunguzi kwenye hafla ya ufunguzi rasmi wa msimu wa uuzaji tumbaku katika Sakafu za Mauzo ya Tumbaku mjini Harare, mji mkuu wa Zimbabwe.
Mwaka huu, uzalishaji wa tumbaku unatarajiwa kupungua kidogo kutokana na ukame unaosababishwa na El Nino, hali ya hewa ya asili na ya mara kwa mara inayopasha joto sehemu za Bahari ya Pasifiki, na kuathiri hali ya hewa. Kutokana na El Nino, msimu wa kilimo ulikuwa na tatizo la kuchelewa kuanza kwa mvua na ukame.
Hekta za ardhi zilizolimwa tumbaku na idadi ya wakulima pia ilipungua kidogo, kwa mujibu wa Bodi ya Viwanda na Uuzaji wa Tumbaku (TIMB), ambayo ni mdhibiti wa sekta hiyo wa nchi hiyo.
Ili kuongeza manufaa yanayotokana na sekta hiyo ya tumbaku yenye hamasa kubwa nchini humo, Chiwenga ametoa wito wa kuongezwa kwa thamani ya ndani ya zao hilo la kibiashara.
"Serikali ina wasiwasi kuwa bado tunauza nje asilimia 98 ya tumbaku yetu ikiwa ghafi, katika mchakato huo tukipeleka nje ya nchi ajira na thamani. Tunahitaji kutengeneza ajira hapa Zimbabwe. Tunatakiwa kuongeza thamani ya mazao yetu," amesema Chiwenga.
Amesema serikali inaweka mazingira wezeshi kwa vyombo vinavyopenda kuongeza thamani ya tumbaku ya Zimbabwe katika mfumo mpana wa uchumi unaoongozwa na sekta binafsi.
Tumbaku ya nchi hiyo inajulikana duniani kote, ikichangia kwa kiasi kikubwa katika mapato ya fedha za kigeni nchini humo, ikiingiza dola za Kimarekani karibu bilioni 1 katika mapato ya mauzo ya nje, kwa mujibu wa TIMB.
Mwaka huu belo la kwanza la zao hilo la “jani la dhahabu” lilipigwa mnada kwa dola 4.92 kwa kilo ikilinganishwa na dola 4.35 mwaka jana.?
Wafanyakazi wa eneo la mnada wa tumbaku wakionekana kwenye hafla ya ufunguzi wa msimu wa uuzaji tumbaku kwa Mwaka 2024 huko Harare, Zimbabwe, Machi 13, 2024. (Picha na Shaun Jusa/Xinhua)
Wafanyakazi wa eneo la mnada wa tumbaku wakionekana kwenye hafla ya ufunguzi wa msimu wa uuzaji tumbaku kwa Mwaka 2024 huko Harare, Zimbabwe, Machi 13, 2024. (Picha na Shaun Jusa/Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma