Lugha Nyingine
Kenya yaanza kutoa motisha kwa wawekezaji wa kigeni katika maeneo maalum ya viwanda
Katibu Mkuu wa Idara ya Taifa ya Viwanda katika Wizara ya Uwekezaji, Biashara na Viwanda ya Kenya Juma Mukhwana amesema siku ya Jumanne kuwa Kenya imeanza kutoa motisha kwa wawekezaji wa kigeni wanaoanzisha biashara katika maeneo maalum ya viwanda.
Bw. Mukhwana amesema hayo kwenye kongamano la biashara lililofanyika mjini Nairobi nchini Kenya, akiongeza kwamba wawekezaji wa kimataifa watapata faida za kodi, pamoja na kupata ardhi bure na mabanda ya viwanda, ili kuwezesha uzalishaji wa bidhaa kwa ajili ya soko la ndani na nje ya nchi.
Mukhwana ameyasema hayo kwenye Maonyesho ya Propak ya Afrika Mashariki 2024, ambayo ni maonyesho na mkutano wa Afrika Mashariki kuhusu vifungashio, na kuongeza kuwa malighafi zitakazotumika katika maeneo hayo maalum ya viwanda pia zitaagizwa bila kutozwa ushuru.
Amesema maeneo hayo yatatoa umeme wa gharama nafuu kwa wazalishaji. Ameongeza kuwa ujenzi wa maeneo 18 ya kaunti na maeneo maalum ya viwanda unaendelea nchini kote, na vituo hivi vinatarajiwa kuwezesha ongezeko la thamani ya malighafi zinazopatikana nchini humo.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma