Lugha Nyingine
Rais Xi Jinping ampongeza Zardari kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Pakistan
BEIJING - Rais Xi Jinping wa China siku ya Jumapili alimpongeza Asif Ali Zardari kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Pakistan akisema China na Pakistan ni majirani wema, marafiki wazuri, washirika wazuri na ndugu wema, huku akiongeza kuwa urafiki ulio kama nguzo ngumu ya chuma kati ya nchi hizo mbili ni chaguo la kihistoria na mali yenye thamani ya watu wa pande hizo mbili.
Rais Xi ameeleza kuwa katika miaka ya hivi karibuni nchi hizo mbili zimedumisha mawasiliano ya karibu kwenye ngazi ya juu, zimeungana mkono katika masuala yanayohusu maslahi yao ya kimsingi na yanayofuatiliwa na pande zote, kupata matokeo mengi katika ujenzi wa Ukanda wa Kiuchumi wa China na Pakistan, na kudumisha maendeleo ya kiwango cha juu ya uhusiano wa pande mbili.
Rais Xi amesema, Dunia inakabiliwa na mabadiliko ya kasi ambayo hayajapata kuonekana katika miaka 100 iliyopita, na umuhimu wa kimkakati umekuwa dhahiri zaidi katika uhusiano wa China na Pakistan.
Kiongozi huyo wa China amesema anathamini sana maendeleo ya uhusiano kati ya China na Pakistan, na angependa kufanya juhudi pamoja na Rais Zardari katika kuendeleza urafiki wa jadi kati ya China na Pakistan, kuendeleza ushirikiano wenye matokeo halisi katika sekta mbalimbali, kusukuma mbele maendeleo makubwa zaidi ya uhusiano wa wenzi wa ushirikiano wa kimkakati wa siku zote kati ya China na Pakistan, kuharakisha ujenzi wa jumuiya iliyo karibu zaidi ya China na Pakistan yenye mustakabali wa pamoja katika zama mpya, ili kunufaisha zaidi watu wa pande hizo mbili.?
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma