Lugha Nyingine
Sarafu ya Zimbabwe yazidi kuporomoka dhidi ya dola ya Marekani
Mfanyabiashara wa sarafu akihesabu pesa mtaani mjini Harare, Zimbabwe, Januari 16, 2024. T (Xinhua/Tafara Mugwara)
HARARE - Gharama za bidhaa na huduma zinaendelea kuongezeka nchini Zimbabwe huku sarafu ya nchi hiyo ikiporomoka thamani dhidi ya dola ya Marekani, hali ambayo iliongezeka mwanzoni mwa Mwaka 2024 ambapo kwa mujibu wa taarifa mpya ya viwango vya ubadilishaji sarafu vya kila siku vya Benki Kuu ya Zimbabwe, dola ya Zimbabawe ambayo iliuzwa kwa 6,192 dhidi ya dola 1 ya Marekani, Januari 2 katika masoko rasmi, sasa inauzwa kwa 8,746 dhidi ya dola hiyo 1 ya Marekani kufikia Januari 17.
Katika soko haramu la sarafu, ambapo Wazimbabwe wengi hununua fedha za kigeni, dola 1 ya Kimarekani inaweza kufikia hadi dola 13,000 za Zimbabwe.
Mchumi Prosper Chitambara amesema thamani ya sarafu ya Zimbabwe ilianza kuporomoka kwa kasi baada ya kutangazwa kwa bajeti ya taifa ya Mwaka 2024 mwishoni mwa mwaka jana na Waziri wa Fedha wa Zimbabwe, Mthuli Ncube.
"Nadhani haikupokelewa vizuri, haswa hatua za ushuru ambazo zilitangazwa na waziri, kwa hivyo imani ya watu kuhusu uchumi inashuka, na tuliona thamani ya sarafu ya hiyo ikiathiriwa, na mwenendo huo pia umeendelea hadi mwaka huu," Chitambara ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Shirikisho la Taifa la Wafanyabiashara la Zimbabwe Christopher Mugaga amesema kushuka kwa thamani ya sarafu huenda kunasababishwa na ukwasi unaoingizwa na serikali kulipia huduma na wakandarasi tofauti.
Watu wakipita duka la pembezoni mwa barabara mjini Harare, Zimbabwe, Januari 16, 2024. (Xinhua/Tafara Mugwara)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma