Lugha Nyingine
Nchi za Afrika Mashariki zatafuta kuongeza watalii wanaowasili katika eneo hilo
KFatuma Albine (Kulia), afisa kutoka Burundi, akitangamana na wageni katika siku ya kwanza ya maonyesho ya utalii yanayofanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Kenyatta (KICC) jijini Nairobi, Kenya, Novemba 20, 2023. (Picha na Fred Mutune/ Xinhua)
NAIROBI - Nchi saba wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumatatu zimeahidi kuboresha sera na mifumo ya usimamizi ili kuongeza watalii wanaowasili baada ya janga la UVIKO-19.
Wakizungumza katika maonyesho ya tatu ya utalii ya kanda ya Afrika Mashariki yanayoendelea Nairobi, Kenya, maafisa waandamizi wameangazia uwezo wa kifursa wa ukuaji wa sekta hiyo, wakitaja wingi na uanuai wa vivutio vya mandhari.
Washiriki zaidi ya 3,000, wakiwemo mawaziri, viongozi wa sekta hiyo na wawekezaji, wanahudhuria maonyesho hayo, yanayoendelea hadi kesho Alhamisi na kuhusisha maonyesho, semina na mitandao ya biashara.
Alfred Mutua, Waziri wa Utalii na Wanyamapori wa Kenya, amesema kuwa nchi wanachama wa EAC zinapaswa kutumia masoko yaliyolengwa na bidhaa mbalimbali ili kuchochea ukuaji katika sekta ya utalii na ukarimu.
Waziri wa Utalii na Wanyamapori wa Kenya Alfred Mutua akizungumza kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Kenyatta (KICC) jijini Nairobi, Kenya, Novemba 20, 2023. (Picha na Fred Mutune/ Xinhua)
"Kama kanda, tunahitaji kuwekeza rasilimali za ziada katika kukuza utalii wa kikanda. Maonyesho haya yanatoa jukwaa la kuendeleza mjadala kuhusu jinsi tunavyoonyesha vizuri zaidi vivutio vya utalii vya kanda kwa wasafiri wa ndani na nje ya nchi," Mutua amesema.
Peter Mathuki, Katibu Mkuu wa EAC, amesema kuwa idadi ya watalii imekuwa kwenye mkondo wa ukuaji katika Jumuiya hiyo, na ikirekodi watalii milioni 7.2 waliofika Mwaka 2019, na makadirio yanalenga kuongeza idadi hiyo hadi kufikia milioni 14.05 ifikapo Mwaka 2025.
"Kufuatia juhudi nyingi za nchi wanachama wa EAC, na katika ngazi ya kikanda, sasa tunaona dalili nzuri za kufufuka kikamilifu kwa utalii," Mathuki amesema.
Amezitaka nchi mbalimbali zioneshe vivutio vya kanda hiyo ambavyo ni fukwe za mchanga za Bahari ya Hindi, milima yenye theluji, mbuga, misitu minene ya mvua, wanyamapori na urithi wa kitamaduni ili kuvutia wageni wengi zaidi.
Mathuki amesisitiza kwamba utekelezaji wa mkakati wa kutangaza utalii wa kikanda unaoanzia Mwaka 2021 hadi 2025 uko kwenye mwelekeo mzuri, akiongeza kuwa michezo, utamaduni na utalii wa kilimo, kama itatumika kikamilifu, inaweza kuongeza watalii wanaofika.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma