Lugha Nyingine
Maonyesho ya mnyororo wa ugavi ya China yavutia waonyeshaji wa kimataifa
Picha hii ya angani iliyopigwa Novemba 7, 2023 ikionyesha bidhaa na magari yanayosubiria kusafirishwa nje ya nchi kwenye bandari kavu ya Horgos mjini Horgos, katika Mkoa unaojiendesha wa Kabila la Wauygur wa Xinjiang, Kaskazini-Magharibi mwa China. (Xinhua/Li Xin)
Beijing - Maonyesho ya kwanza ya Kimataifa ya Mnyororo wa Ugavi ya China (CISCE), ambayo yatazinduliwa Novemba 28, yatavutia washiriki zaidi ya 1,000, wakiwemo wawakilishi kutoka idara za serikali, jumuiya za wafanyabiashara, mashirika ya kimataifa, wataalam na wasomi, kwa mujibu wa mkutano na waandishi wa habari wa siku ya Jumanne.
Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Kuhimiza Biashara ya Kimataifa la China Zhang Shaogang amesema kampuni na taasisi 515 za China na nchi za nje zitashiriki katika maonyesho hayo mjini Beijing, na nyingi tayari zimetenga maeneo ya maonyesho kwa ajili ya maonyesho ya pili.
Maonyesho haya ya mwaka huu yatahusisha shughuli mbalimbali zaidi ya 20, zikiwemo za ufafanuzi wa sera, mabadilishano na majadiliano, mazungumzo, utangazaji wa kutoa bidhaa mpya, kati ya mada nyingine.
Yakiwa na eneo la maonyesho lenye ukubwa wa mita za mraba zaidi ya 100,000, maonyesho hayo yatakuwa na maeneo yaliyowekwa maalum kwa ajili ya minyororo ya ugavi kwa magari yanayotumia teknolojia ya kisasa, kilimo cha kijani, nishati safi, maisha yenye afya na teknolojia za kidijitali.
Maonyesho ya CISCE, ambayo ni maonesho ya kwanza duniani ya kiwango cha kitaifa ya ugavi, yanatazamiwa kufanyika Beijing kuanzia Novemba 28 hadi Desemba 2, yakiwa na kaulimbiu isemayo "Kuunganisha Dunia kwa Mustakabali wa Pamoja."?
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma