Lugha Nyingine
Mwalimu wa Tanzania awawezesha vijana kwa ujuzi wa lugha ya Kichina
Asha Fum Khamis, mwalimu wa lugha ya Kichina kutoka Tanzania Zanzibar katika Taasisi ya Confucius ndani ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, akizungumza wakati alipohojiwa na Shirika la Habari la China, Xinhua jijini Dar es Salaam, Tanzania, Novemba 17, 2023. (Picha na Herman Emmanuel/Xinhua)
DAR ES SALAAM - "Lugha ya Kichina ni lugha ya duniani kote katika siku hizi. Ni lugha inayofungua fursa kwa vijana, nchini Tanzania na dunia nzima," amesema Asha Fum Khamis, mwalimu wa lugha ya Kichina kutoka Tanzania Zanzibar katika Taasisi ya Confucius ndani ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Tanzania.
Akitoa maoni yake zaidi, mwalimu huyo mwenye umri wa miaka 32 amesema "Natamani babu na bibi yangu, wazazi wangu na ndugu zangu wajifunze lugha ya Kichina kwa sababu huo ndiyo ufunguo wa kupata ajira katika kampuni za China zinayofanya kazi nchini Tanzania." Ametoa maoni haya muda mfupi baada ya kumaliza kufundisha darasa la lugha ya Kichina katika Taasisi ya Confucius siku ya Ijumaa asubuhi.
Asha, mwenye mume Mtanzania anayejua vizuri lugha ya Kichina na ana mtoto wa kiume wa miezi sita, amesema kwa fahari kwamba ameshafundisha Lugha ya Kichina kwa wanafunzi Watanzania zaidi ya 300 katika miaka yake mitatu ya ualimu. "Takriban wanafunzi 50 kati yao niliowafundisha wameajiriwa kuwa walimu wa lugha ya Kichina na baadhi ya wengine wamepata kazi za staha za wakalimani katika kampuni za China zilizoko Tanzania."
Akisisitiza ongezeko la mahitaji ya wazungumzaji wa lugha ya Kichina, Asha amesema "karibu kila siku, maofisa kutoka kampuni za China zinazofanya kazi nchini Tanzania wanafika katika Taasisi ya Confucius kutafuta Watanzania wenye ujuzi wa Lugha ya Kichina."
Taasisi ya Confucius katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, iliyoadhimisha miaka 10 tangu kuanzishwa kwake Julai 2023, imekuwa na jukumu muhimu katika kuongeza mabadilishano ya kitamaduni na mafunzo ya lugha ya Kichina, na kuchangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha uhusiano kati ya China na Tanzania.
"Wazungumzaji wa lugha ya Kichina wanahitajika sana siyo tu nchini Tanzania na Afrika lakini pia duniani kote ambapo kampuni zinazohusiana na China zinafanya kazi," anaendelea, huku akitaja kwamba tayari ameanza kumfundisha mtoto wake wa kiume Lugha ya Kichina, ingawa hana uhakika kama anaelewa lugha hiyo.
Upendo wake wa lugha ya Kichina bila kutarajiwa ulianza wakati akiwa Chuo cha Uandishi wa Habari na Vyombo vya Habari Zanzibar Mwaka 2013, ambapo mwanafunzi mwenzake alizungumza kwa ufasaha na walimu wa China. Alianza kujifunza Lugha ya Kichina kuanzia Mwaka 2013 hadi 2016, na kupata diploma ya uandishi wa habari.
Asha Fum Khamis, mwalimu wa lugha ya Kichina kutoka Tanzania Zanzibar katika Taasisi ya Confucius ndani ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, akifundisha lugha ya Kichina jijini Dar es Salaam, Tanzania, Novemba 17, 2023. (Picha na Herman Emmanuel/Xinhua)
Asha Fum Khamis, mwalimu wa lugha ya Kichina kutoka Tanzania Zanzibar katika Taasisi ya Confucius ndani ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, akizungumza na mwanafunzi wakati wa darasa la lugha ya Kichina jijini Dar es Salaam, Tanzania, Novemba 17, 2023. (Picha na Herman Emmanuel/Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma