Lugha Nyingine
Mnada wa chai kupiga jeki biashara Tanzania
Wakati Tanzania ikianza kufanya mnada wa kwanza wa zao la chai katika jengo la Millennium Towers jijini hapa, matumaini makubwa yamekuwepo, ambapo tani 57 zinatarajiwa kuuzwa katika tukio hilo la kihistoria.
Mnada huo uliofanyika Novemba 13 kwa kupewa baraka na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Gerald Mweli, unatarajiwa kuongeza matumizi na shughuli zinazofanywa katika bandari za Dar es Salaam na Tanga pamoja na kuongeza uwazi katika biashara ya chai nchini Tanzania.
Kwa muda mrefu minada ya chai imekuwa ikifanyika nchini Kenya, nchi mbayo pia ni mzalishaji mkubwa wa zao hilo barani Afrika.
Akizungumza na wanahabari, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Chai, Mary Kipeja, amesema mnada huo utaifanya Tanzania kuwa kituo cha biashara ya chai katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Amesema uanzishwaji wa mnada huo utapunguza gharama kwa asilimia 50, ikilinganishwa na kiasi kilichotumika kusafirisha bidhaa hiyo hadi Mombasa nchini Kenya kwa mauzo.
Amesema kupitia bandari za Dar es Salaam na Tanga zitakazotumika kusafirisha bidhaa iliyouzwa mnadani, Serikali itaongeza mapato na kuzalisha ajira kwa wananchi.
Amesema wasindikaji 10 wametia saini mikataba ya kushirikiana na madalali, wengine saba wanaendelea na mazungumzo na kwamba wanunuzi tisa waliosajiliwa wanatarajiwa kushiriki katika minada ya zao hilo.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma