Lugha Nyingine
Waziri Mkuu wa China Li Qiang asisitiza kufungua mlango zaidi
Waziri Mkuu wa China Li Qiang akihudhuria hafla ya ufunguzi wa Maonyesho ya sita ya Kimataifa ya Uagizaji Bidhaa ya China (CIIE) na Baraza la Uchumi la Kimataifa la Hongqiao na kutoa hotuba kuu mjini Shanghai, Mashariki mwa China, Novemba 5, 2023. (Xinhua/Zhai Jianlan)
SHANGHAI - Waziri Mkuu wa China Li Qiang amesisitiza juhudi za kupanua zaidi ufunguaji mlango wa China na kuchangia fursa za maendeleo za China na Dunia nzima wakati akitoa hotuba yake kuu kwenye hafla ya ufunguzi wa Maonyesho ya sita ya Kimataifa ya Uagizaji Bidhaa ya China (CIIE) na Baraza la Uchumi la Kimataifa la Hongqiao siku ya Jumapili mjini Shanghai.
China itaendelea kuhimiza ufunguaji mlango na fursa kubwa zaidi za soko, Waziri Mkuu Li amesema, huku akiongeza kuwa China ina idadi ya watu zaidi ya bilioni 1.4 na kundi la watu wenye kipato cha kati zaidi ya milioni 400, inatoa fursa kubwa kutokana na mahitaji ya soko.
Huku akibainisha kuwa China siku zote iko tayari kuchangia fursa zake za soko, Waziri Mkuu Li amesema nchi hiyo itapanua kikamilifu uagizaji wa bidhaa kutoka nje, itahimiza maendeleo yaliyoratibiwa ya biashara ya bidhaa na ya huduma, kutekeleza orodha hasi za biashara ya huduma za kuvuka mpaka, kuunga mkono uvumbuzi katika miundo na mifano ya biashara ya nje, na kukuza biashara ya kidijitali.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Li, uagizaji wa bidhaa na huduma wa China kutoka nje unatarajiwa kufikia dola trilioni 17 za Kimarekani kwa jumla katika miaka mitano ijayo.
Amesisitiza kuwa China itaendelea kurahisisha ufikiaji wa soko na kutekeleza sera ili kuondoa vikwazo vyote vya uwekezaji wa kigeni katika sekta ya viwanda.
“China italinda haki na maslahi ya wawekezaji wa kigeni kwa mujibu wa sheria, na kuendelea kuweka mazingira ya biashara ambayo yana mwelekeo wa soko, yanayozingatia sheria na kufikia viwango vya kimataifa,” amesema Waziri Mkuu Li.
Amesema China iko tayari kuongeza ushirikiano na nchi zote katika uvumbuzi, kuwezesha muunganisho wa pande zote wa sayansi na teknolojia pamoja na uchumi, kuhamasisha kunufaishana matokeo ya uvumbuzi, na kujitahidi kuondoa vikwazo vinavyozuia mtiririko wa ujuzi, teknolojia, vipaji na mambo mengine ya uvumbuzi.
Waziri Mkuu wa China Li Qiang akitembelea mabanda ya maonyesho pamoja na viongozi wa kigeni baada ya hafla ya ufunguzi wa Maonyesho ya sita ya Kimataifa ya Uagizaji Bidhaa ya China (CIIE) na Baraza la Uchumi la Kimataifa la Hongqiao mjini Shanghai, Mashariki mwa China, Novemba 5, 2023. (Xinhua/Pang Xinglei)
Waziri Mkuu wa China Li Qiang akitembelea banda la maonyesho kabla ya hafla ya ufunguzi wa Maonyesho ya sita ya Kimataifa ya Uagizaji Bidhaa ya China (CIIE) na Baraza la Uchumi la Kimataifa la Hongqiao mjini Shanghai, Mashariki mwa China, Novemba 5, 2023. (Xinhua/Pang Xinglei)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma