Lugha Nyingine
Maonesho ya 134 ya Canton yanaanza mjini Guangzhou
Maonesho ya 134 ya Uagizaji na Mauzo ya Nje ya China, ambayo yanajulikana kama ‘Canton Fair’, yalifunguliwa Jumapili huko Guangzhou, mji mkuu wa Mkoa wa Guangdong kusini mwa China. Maonesho haya yatakayoendelea hadi Novemba 4, yamevutia waoneshaji na wanunuzi kutoka kote duniani. Msemaji wa maonesho hayo Xu Bing amesema, zaidi ya wanunuzi 100,000 kutoka zaidi ya nchi na maeneo 200 wamejiandikisha kwa ajili ya tukio hilo. Ameelza kuwa jukwaa la mtandaoni la maonesho hayo litatoa huduma kwa waoneshaji na wanunuzi.
Yakilinganishwa na maonesho yaliyopita, eneo la maonesho ya mwaka huu limepanuliwa kwa mita za mraba 50,000 na idadi ya mabanda ya maonesho pia itaongezeka kwa karibu 4,600.
Zaidi ya waoneshaji 28,000 watashiriki katika maonesho hayo , ikijumuisha biashara 650 kutoka nchi na maeneo 43. Maonesho hayo yaliyoanzishwa mwaka 1957 na kufanyika mara mbili kwa mwaka, yanachukuliwa kuwa kipimo kikuu cha biashara ya nje ya China.
Wakati huohuo zaidi ya wafanyabiashara 95 wa Tanzania watashiriki kwenye maonesho ya mafunzo ya wajasiliamali katika maonesho hayo ya ‘Canton Fair’ kupitia Chama cha Wafanyabiashara Wanawake Tanzania.
Akifafanua zaidi juu ya safari hiyo, Mkurugenzi wa TWCC, Mercy Sila amesema lengo la safari hiyo ni kuwawezesha wajasiliamali hao kupata fursa za kimataifa, ambapo wataweza kujionea mashine za viwanda, vipodozi, mavazi, mashine za kilimo au mashine za kutengeneza chakula. Alisema mategemeo makubwa ya safari hiyo ni kuhakikisha kwamba wafanyabiashara hao wakirudi watakuwa sio sawa na wale walioondoka, kwakuwa biashara zao zitakua na kuchangia katika kukua kwa uchumi.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma