Lugha Nyingine
Mkoa?wa Jiangxi wa China wafanya kongamano la kukuza biashara?na?uwekezaji nchini Kenya
NAIROBI - Kenya Jumatatu ilikuwa mwenyeji wa kongamano la kukuza uwekezaji na biashara la Mkoa wa Jiangxi wa China katika mji mkuu wa Nairobi, huku washiriki wakiwemo maafisa waandamizi, wanadiplomasia na wawekezaji wakitoa wito wa kuimarishwa kwa uhusiano wa kiuchumi kati ya China na Kenya.
Kongamano hilo lililoandaliwa na Shirikisho la Taifa la Biashara na Viwanda la Kenya (KNCCI), limejadili ushirikiano katika sekta muhimu kama vile viwanda, nishati safi, huduma za afya, utalii, madini na teknolojia ya habari na mawasiliano.
Likiwa limefanyika kwa siku moja, kongamano hilo lilibeba kaulimbiu isemayo "Kukuza ushirikiano wa kirafiki na kuhimiza ustawi wa pamoja" na kusisitiza haja ya kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya China na Kenya kuendana na Pendekezo la Ukanda Mmoja, Njia Moja. Washiriki wametoa wito wa kuundwa kwa jukwaa la kuongeza uchangiaji wa maarifa na uhamishaji wa teknolojia miongoni mwa wawekezaji wa China na Kenya ili kupata manufaa ya pamoja ya kijamii na kiuchumi.
Abubakar Hassan Abubakar, Katibu Mkuu wa Idara ya Serikali ya Kenya ya Kukuza Uwekezaji, amesema kuwa Kenya ina nia ya kuimarisha biashara inayoongezeka na China ili kuharakisha maendeleo ya uchumi.
"Kenya iko wazi kwa biashara na kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji kati yake na China kutafungua ustawi wa pamoja," Abubakar amesema, huku akiongeza kuwa serikali ya Kenya imeondoa vikwazo vya usimamizi ili kuwezesha uwekezaji wa China katika sekta za viwanda, huduma za kifedha, kilimo na utalii.
Kwenye kongamano hilo, ukiacha mikataba mbalimbali ya kibiashara iliyosainiwa, makubaliano ya maelewano yametiwa saini kati ya KNCCI na Kamati ya Mkoa wa Jiangxi ya Baraza la China la Kukuza Biashara ya Kimataifa.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma