Lugha Nyingine
Treni za muundo wa kuunganisha reli na bahari za China zafanya safari 30,000 tangu kuzinduliwa
Picha iliyopigwa Oktoba 2, 2023 ikionyesha eneo la kuhifadhia makontena kwenye Bandari ya Qinzhou huko Qinzhou, Mkoa unaojiendesha wa Kabila la Wazhuang wa Guangxi, Kusini mwa China. (Xinhua/Zhang Ailin)
NANNING - Treni za muundo wa kuunganisha reli na bahari za China zimefanya safari zaidi ya 30,000 kwenye Ukanda Mpya wa Kimataifa wa Biashara ya Nchi Kavu na Baharini tangu huduma hiyo ilipoanza Mwaka 2017, imesema serikali ya Mkoa unaojiendesha wa Kabila la Wazhuang wa Guangxi, Kusini mwa China siku ya Jumapili.
Siku ya Jumapili, treni ya muundo wa kuunganisha reli na bahari iliyobeba makontena 110 yenye bidhaa mbalimbali iliondoka kutoka kituo cha makontena cha reli cha Qinzhou huko Guangxi. Ikiwa inaelekea Mji wa Chongqing, Kusini-Magharibi mwa China, treni hiyo inatimiza idadi ya safari ya 30,000.
Ukiwa ulizinduliwa Mwaka 2017, Ukanda Mpya wa Kimataifa wa Biashara ya Nchi kavu na Baharini ni njia ya biashara na uchukuzi iliyojengwa kwa pamoja na maeneo ya ngazi ya mkoa wa magharibi mwa China na nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Asia Kusini Mashariki (ASEAN). Tangu ukanda huo ulipozinduliwa, treni zake za muundo wa kuunganisha reli na bahari zimerekodi idadi inayoongezeka ya safari na ongezeko la kila mwaka la mizigo.
Bidhaa nyingi zaidi za kilimo kutoka ASEAN na nchi nyingine, kama vile mchele wa Cambodia, nazi za Thailand, na nyama iliyogandishwa ya Brazil, zimeingia kwenye soko la China kupitia ukanda huo. Wakati huo huo, bidhaa za nishati mpya za China, nyenzo mpya, na bidhaa za mitambo na umeme zinasafirishwa nje ya nchi kupitia ukanda huo, amesema Li Hongfeng kutoka Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya Usafirishaji wa Ghuba la Guangxi.
Hivi sasa, ukanda huo unatoa huduma zinazojumuisha vituo 138 katika miji 69 ya maeneo 18 ya ngazi ya mkoa nchini China.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma