Lugha Nyingine
Tanzania yakaribisha wawekezaji zaidi wa China kuunga mkono maendeleo ya viwanda
Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa (kushoto) akipeana mkono na Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian kwenye Jukwaa la Uwekezaji la China-Tanzania na Mkutano wa Biashara na Uwezekaji wa Mkoa Zhejiang (Jinhua) na Tanzania jijini Dar es Salaam, Tanzania, Septemba 25, 2023. (Picha na Emmanuel Herman/Xinhua)
DAR ES SALAAM - Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema kwamba nchi hiyo imefungua milango yake kwa wawekezaji zaidi wa China kuunga mkono mikakati ya nchi hiyo ya maendeleo ya viwanda.
"Tanzania iko tayari kufanya biashara nanyi; milango yetu iko wazi," Majaliwa amewahakikishia wawekezaji hao kutoka China wakati akifunga shughuli ya siku moja ya Jukwaa la Uwekezaji la China-Tanzania na Mkutano wa Biashara na Uwezekaji wa Mkoa Zhejiang (Jinhua) na Tanzania iliyofanyika Jumatatu jijini Dar es Salaam.
Ameongeza kuwa Tanzania ina mazingira mazuri ya biashara, sera nzuri za kiuchumi, utulivu wa uchumi mkuu, maliasili nyingi, nguvu kazi iliyoelimika, na soko kubwa kwa sababu ya eneo la kipekee la kijiografia la nchi hiyo.
Jukwaa hilo limevutia zaidi ya wawakilishi 100 wa sekta ya uchumi na biashara wakiongozwa na Baraza la China la Kukuza Biashara ya Kimataifa (CCPIT) Kamati ya Mkoa wa Zhejiang na Serikali ya Mji wa Jinhua katika Mkoa wa Zhejiang, Mashariki mwa China.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais anayeshughulikia Mipango na Uwekezaji Kitila Mkumbo amewataka wawekezaji wazawa kuungana na wenzao wa China ili kujenga msingi imara wa viwanda nchini Tanzania.
Mkumbo amesema ajenda ya Tanzania ya viwanda inaweza kutekelezwa kwa kualika na kuvutia wawekezaji wengi kutoka sehemu mbalimbali za Dunia hususani China.
Kwa upande wake Chen Mingjian, Balozi wa China nchini Tanzania, amesema Tanzania, ikiwa ni moja ya nchi zenye uchumi unaokua kwa kasi barani Afrika, imefanya kuvutia uwekezaji na mitaji ya kigeni kuwa lengo muhimu la sera ya uchumi.
Chen amesema kampuni za China zinaiona Tanzania kama sehemu ya kuleta maendeleo na ukuaji wa kiuchumi wa pande zote mbili, akiongeza kuwa kampuni nyingi za China zinaichukulia Tanzania kama msingi muhimu wa uzalishaji, zikisafirisha bidhaa katika nchi mbalimbali za Afrika kutoka nchi hiyo, na kutoa ajira kwa watu zaidi ya 150,000 nchini Tanzania.
Ujumbe huo wa China ulikuja na nia ya kuwekeza katika nyanja mbalimbali, ikiwa ni pamoja na dawa na vifaa tiba, uzalishaji wa chakula, mashine za kilimo, bidhaa za kilimo, uchukuzi, mashine na vifaa vya ujenzi, malighafi za aluminia na shaba na mengine mengi.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma