Lugha Nyingine
Afrika Kusini yasaini makubaliano ya kuuza parachichi China
Mauzo ya bidhaa nje ya nchi ya Afrika Kusini yamepata kichocheo wakati nchi hiyo iliposaini makubaliano ya kuuza parachichi China.(Picha kutoka CFP))
Jumanne ya wiki iliyopita, Waziri wa Kilimo, Mageuzi ya Ardhi na Maendeleo Vijijini wa Afrika Kusini, Thoko Didiza, alisaini makubaliano na Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi, wakati Rais wa China Xi Jinping alipofanya ziara rasmi Afrika Kusini. Didiza alisema amefurahi kusaini makubaliano hayo, ambayo yatatengeneza ajira zaidi nchini na kukuza uchumi.
"Kupata fursa ya kuingia China ni hatua muhimu katika kuchochea ukuaji unaongozwa na mauzo ya nje ya parachichi ya Afrika Kusini, ambayo ni ahadi serikali imetoa chini ya mpango mkuu wa kilimo na usindikaji wa mazao," amesema Didiza.
Didiza amesema kuuza parachichi China kutaifanya Afrika Kusini kupanda na kuzalisha matunda zaidi, hususan parachichi, na kuongeza fursa za ajira. China inatarajiwa kuwa moja ya masoko makubwa ya parachichi duniani na hilo linatoa fursa kubwa kwa Afrika Kusini, amesema.
Wakati huo huo, Chama cha Wakulima wa Matunda Jamii ya Machungwa cha Afrika Kusini kimesema mauzo ya matunda hayo kwa China yalifikia tani 477,974 Mwaka 2022.
Wandile Sihlobo, mchumi mkuu wa Shirikisho la Biashara za Kilimo la Afrika Kusini, amekaribisha kufunguliwa kwa soko la China kwa parachichi kutoka Afrika Kusini.
"Nchi za BRICS ni soko muhimu la kilimo kwa sababu ukizifikiria kwa vigezo vya thamani, hili ni soko lenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 300. Bila shaka, China ni soko muhimu ikichangia thuluthi mbili ya mchango huo," amesema.
Biashara kati ya China na Afrika Kusini imepiga hatua kubwa kutoka dola bilioni 1.4 mwaka 1998 hadi dola bilioni 56.7 mwaka 2022, kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma