Lugha Nyingine
Sarafu ya China yazidi kupata umaarufu wakati kukiwa na ongezeko la uhusiano wa kibiashara kati ya China na Kenya
Ofisa mkuu mtendaji wa Chama cha Mabenki cha Kenya (KBA) Bw. Habil Olaka, amesema sarafu ya China, renminbi au Yuan, inaendelea kupata umaarufu miongoni mwa wakopeshaji wa kibiashara kutokana na kuongezeka kwa mahusiano ya kibiashara kati ya China na Kenya.
Bwana Olaka ameliambia shirika la habari la China Xinhua mjini Nairobi, kuwa renminbi imeanza kuwa sarafu mbadala ya dola ya Marekani katika kufanya miamala ya kifedha inayohusisha biashara kati ya Kenya na China.
Akiongea kwenye hafla ya kutolewa kwa ripoti kuhusu Uchangiaji wa Kodi ya Jumla wa Sekta ya Benki ya Kenya kwa 2022 iliyoandaliwa na KBA, Bw. Olaka amesema kinachoelekea kutokea kati ya nchi hizo mbili zinazofanya biashara, ni kutumia sarafu inayopatikana kwa urahisi katika nchi zao.
Ofisi ya taifa ya Takwimu ya Kenya KBS, imesema mwaka 2022 thamani ya jumla ya mauzo ya nje ya Kenya kwa China imefikia shilingi bilioni 27.5 (sawa na dola milioni 193) huku thamani ya uagizaji wa bidhaa kutoka China ikifikia dola bilioni 3.17. Takwimu za serikali zinaonyesha kuwa China imekuwa mshirika mkubwa zaidi wa kibiashara, mwekezaji mkubwa wa kigeni na mkandarasi mkubwa wa mradi kwa Kenya.
Bw. Olaka pia amesema kwa sasa benki nyingi za biashara zina kitengo cha biashara cha Yuan ambacho hufanya sarafu ya China kupatikana ndani ya nchi. Amesema matumizi ya sarafu inayofaa ni jambo muhimu katika kuhimiza biashara kati ya nchi hizo mbili, akibainisha kuwa benki za Kenya zinakubaliana na matumizi ya Yuan katika biashara kati ya China na Kenya, kwa sababu inapunguza gharama kubadilisha sarafu kuwa dola ya Marekani.
Pia amesema benki nyingi zinazofanya kazi nchini Kenya pia zimefungua madawati ya lugha ya Kichina ili kuhudumia jumuiya ya wafanyabiashara wa China inayoendelea kuongezeka nchini Kenya.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma