Lugha Nyingine
Mfumo Unganishi wa Kifedha kati ya Hong Kong na China Bara wazinduliwa rasmi
Picha ya kumbukumbu ikionyesha mwonekano wa nje wa Benki ya Watu wa China hapa Beijing, China. (Xinhua/Peng Ziyang)
BEIJING - Mfumo Unganishi wa Kifedha na Kibiashara, Swap Connect, ambao ni mpango wa kufikia soko la kubadilisha viwango vya riba, umezinduliwa rasmi Jumatatu, kwa mujibu Benki ya Watu wa China (PBOC) ambayo ni Benki Kuu ya China.
Chini ya mfumo huo, wawekezaji wa ndani na nje ya China wataruhusiwa kufanya biashara ya kubadilishana riba za sarafu ya China, renminbi na kushughulikia vibali vya kibiashara kupitia taasisi za miundombinu katika maeneo ya China Bara na Mkoa wa Utawala Maalum wa Hong Kong (HKSAR), PBOC imesema katika taarifa yake ya mtandaoni.
Huku kukiwa na mipango ya kitaasisi ambayo imefanywa katika biashara, kushughulikia vibali na malipo, wawekezaji wataweza kushiriki katika masoko ya bidhaa zinazotokana na fedha ya China Bara na Hong Kong bila kulazimika kubadilisha utendaji wao wa kibiashara uliopo, benki kuu ya China imesema.
Pan Gongsheng, Naibu Gavana wa PBOC amesema wakati akihutubia hafla ya uzinduzi kuwa, kuanzishwa kwa mfumo huo kumeashiria hatua muhimu katika ufunguaji wa sekta ya kifedha ya China na kudhihirisha azma thabiti ya serikali kuu ya China ya kuunga mkono ustawi, utulivu na maendeleo ya muda mrefu ya Hong Kong.
Swap Connect itaimarisha na kuboresha hadhi ya Hong Kong kama kituo cha kifedha cha kimataifa, kutoa njia rahisi zaidi ya kudhibiti hatari za viwango vya riba, na kuhimiza ufunguaji wa sekta ya kifedha ya China kwa kasi, benki kuu hiyo imesema.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma