Lugha Nyingine
Rais Xi Jinping wa China asema mazungumzo ndiyo njia pekee ya kutatua mgogoro wa Ukraine
BEIJING - Rais wa China Xi Jinping amesema Jumatano kwamba mazungumzo na majadiliano ndiyo njia pekee inayoweza kutatua mgogoro wa Ukraine, na kwamba hakuna anayeweza kushinda vita vya nyuklia.
Ametoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na mwenzake wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, kwa njia ya simu. Pande hizo mbili zimebadilishana mawazo kuhusu uhusiano kati ya China na Ukraine na mgogoro wa Ukraine.
Rais Xi amesema China itatuma mjumbe maalum wa serikali ya China ashughulikiaye mambo kuhusu Ulaya na Asia, kutembelea Ukraine na nchi nyingine ili kufanya mawasiliano ya kina na pande zote kuhusu utatuzi wa kisiasa wa mgogoro huo.
Rais Xi ameeleza kuwa uhusiano kati ya nchi hizo mbili umepitia miaka 31 ya maendeleo na kufikia kiwango cha ushirikiano wa kimkakati, jambo ambalo limeongeza maendeleo na ustawishaji wa nchi hizo mbili.
Rais Xi amesema anashukuru kauli za mara kwa mara za Rais Zelensky za kusisitiza kuendeleza uhusiano na ushirikiano kati ya China na Ukraine, na kuishukuru Ukraine kwa kutoa msaada mkubwa kwa ajili ya kuhamisha raia wa China mwaka jana.
"Kuheshimiana kwa mamlaka ya nchi na ukamilifu wa ardhi, ni msingi wa kisiasa wa uhusiano wa nchi mbili" Rais Xi amesema.
Kuhusu mgogoro wa Ukraine, Rais Xi amesema, China siku zote inasimama upande wa amani, na msimamo wake wa msingi ni kuhimiza mazungumzo ya amani.
Amerejea mapendekezo yake ya mambo manne kuhusu nini kifanyike, mambo manne ambayo jumuiya ya kimataifa inapaswa kufanya kwa pamoja na masuala matatu ya kutilia maanani, akisema kuwa kwa msingi huu, China imetoa msimamo wake kuhusu Suluhu ya Kisiasa ya Mgogoro wa Ukraine.
Ameongeza kuwa, China itaendelea kuhimiza mazungumzo ya amani na kufanya juhudi zake katika kusitisha mapigano na kurejesha amani mapema.
“China imetuma shehena nyingi za msaada wa kibinadamu kwa Ukraine na itaendelea kutoa msaada kwa kadiri ya uwezo wake,” Rais Xi amesema.
Kwa upande wake Rais Zelensky pamoja na kumpongeza Rais Xi kwa kuchaguliwa tena, amesema upande wa Ukraine umefuata kwa makini sera ya kuwepo kwa China moja, na ametoa maoni yake kuhusu hali ya sasa ya mgogoro wa Ukraine, huku akiishukuru China kwa kutoa msaada wa kibinadamu kwa Ukraine, na kukaribisha mchango muhimu wa China katika kurejesha amani na kutafuta ufumbuzi wa kidiplomasia wa mgogoro huo.?
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma