Lugha Nyingine
Mashirika na viongozi wa biashara wa kimataifa wajenga matumaini kuhusu mtazamo wa uchumi wa China
Wafanyakazi wakifanya kazi kwenye kiwanda kimoja cha kuunda magari cha Kampuni ya Magari ya Benz iliyoko Beijing, China Februari 21, 2020. (Xinhua/Chen Zhonghao)
BEIJING - Wataalamu wa uchumi na viongozi wa biashara wameonyesha matumaini kuhusu mtazamo wa ukuaji wa uchumi wa China Mwaka 2023 kwenye Mkutano wa Kongamano la Maendeleo la China (CDF) 2023 uliofungwa wiki hii, wakisema kuwa China ni kichocheo kikuu cha uchumi wa Dunia na msambazaji wa kuaminika wa minyororo ya viwanda na utoaji wa bidhaa.
Katika ripoti yake ya kazi ya serikali, China iliweka lengo la ongezeko la uchumi wake kwa karibu asilimia 5 mwaka huu. Kevin Kang, mwanauchumi mkuu wa KPMG China, amesema lengo hilo ni la juu zaidi kuliko makadirio ya ukuaji wa uchumi wa nchi nyingine zenye uchumi mkubwa.
“Sekta ya matumizi ya China inatarajiwa kuharakisha ufufukaji wake, na uvumbuzi wa kiteknolojia na mabadiliko ya kijani ya China yanakuza uwekezaji katika viwanda,” Kang amesema.
Ameongeza kuwa, wakati nchi hiyo ikishika kasi yake ya kufufua uchumi, na huku ukuaji wa uchumi duniani ukishuka, uchumi wa China unatarajiwa kuibuka tena kama kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi wa Dunia.
Zhu Min, Makamu Mwenyekiti wa Kituo cha China cha Mabadilishano ya Kiuchumi ya Kimataifa, anaamini kwamba lengo la ongezeko la asilimia 5 ni la busara na endelevu wakati wa hali ya uchumi wa Dunia kutokuwa na uhakika kuongezeka.
Zhu ametaja mambo kama vile uimarishaji wa soko la mali, ufufukaji wa matumizi na uwekezaji thabiti katika sekta ya viwanda vinavyotumia teknolojia ya hali ya juu, ambayo yote yatachangia kufikia lengo hilo la uchumi kukua kwa asilimia 5.
Ingawa wasomi, wachambuzi na viongozi wengi wa biashara wamezungumza juu ya changamoto nyingi katika mazingira mapana ya uchumi wa Dunia, wamesema pia kuwa China inapaswa kuwa na ujasiri wa kukabiliana na changamoto za nje.
"China tayari imejikita kwa kina katika mnyororo wa thamani wa kimataifa na kuwa kituo cha viwanda vya utengenezaji bidhaa duniani na 'kiwanda cha Dunia,' kutokana na zaidi ya miaka 40 ya mageuzi na kufungua mlango," amesema Yi Xiaozhun, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa zamani wa Shirika la Biashara Duniani (WTO).
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma