Lugha Nyingine
Ziara ya Rais Xi nchini Russia itakuwa ya kirafiki, ushirikiano na amani
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Bw. Wang Wenbin, ametoa ufafanuzi kuhusu ziara atakayofanya Rais Xi Jinping wa China nchini Russia, kuwa kwenye ziara hiyo atabadilishana maoni kwa kina na mwenyeji wake Rais Vladimir Putin wa Russia kuhusu uhusiano kati ya nchi hizo mbili na masuala makubwa ya kimataifa na kikanda yanayofuatiliwa na nchi zao. Pia amesema ziara hiyo inalenga kuhimiza uratibu wa kimkakati wa China na Russia na ushirikiano kati ya nchi hizo mbili katika mambo halisi, na kuleta tija mpya katika ukuaji wa uhusiano kati ya China na Russia.
Msemaji huyo ameongeza kuwa, Dunia inashuhudia mabadiliko makubwa kwa kasi na kuingia katika kipindi kipya chenye misukosuko. Zikiwa ni nchi wajumbe wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, na nchi kubwa zenye ushawishi, uhusiano kati ya China na Russia una maana na nguvu kubwa ya ushawishi ambazo zimezidi nchi hizo mbili zenyewe.
Msemaji huyo pia amesisitiza kuwa, ziara hiyo ya Rais Xi nchini Russia itakuwa ni ziara ya kirafiki, ushirikiano na amani, ambapo China na Russia zinatekeleza ushirikiano wa pande nyingi kwa msingi wa kanuni ya kutofungamana, kutopingana na kutolenga upande wa tatu. Na kuhusu mgogoro wa Ukraine, China inaendelea kushikilia msimamo unaotetea haki na kutoa mchango wa kiujenzi ili kufanikisha mazungumzo na kuleta amani.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma