Lugha Nyingine
Kurejeshwa kwa safari za nje za makundi ya watalii na China kunatarajiwa kufufuka kwa shughuli za utalii duniani
Kundi la watalii wanaomfuata mwongozaji watalii wakikaribia kuanza safari kuelekea Thailand katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Shanghai Pudong huko Shanghai, Mashariki mwa China, Februari 6, 2023. (Xinhua/Chen Aiping)
SHANGHAI – Shughuli za utalii duniani zinatarajiwa kuimarika kwani China, ambayo ni moja ya soko kubwa zaidi la utalii duniani kabla ya janga la UVIKO-19 kulipuka, imerejesha tena safari za nje za makundi ya watalii siku ya Jumatatu.
Huang Xing mwenye umri wa miaka 69 akiwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Shanghai Pudong, alionekana mwenye furaha kubwa, wakati akikaguliwa tiketi na mizigo pamoja na marafiki zake watatu tayari kwa kuanza safari iliyopangwa kwa muda mrefu kwenda Phuket, Thailand
Marafiki hao wamewahi kufanya safari kadhaa za nje ya nchi pamoja kabla ya janga la korona, na sasa wanapanga pia safari ya kwenda Ulaya Mashariki baadaye mwaka huu.
"Thailand iko karibu, na ingawa ni safari ya kundi, ratiba imetulia na ni vizuri kuwa na marafiki," amesema Huang.
Huang ni miongoni mwa kundi la watalii 25 katika safari yao ya kuelekea Thailand iliyoandaliwa na Kampuni ya Kimataifa ya Shanghai Airlines Tours.
Tangu Jumatatu wiki hii, China imetangaza kurejesha safari za makundi ya watalii katika nchi 20, zikiwemo Thailand, Maldives, Falme za Kiarabu, Russia na New Zealand.
Hatua hiyo, iliyotangazwa Januari, ilizua shauku kubwa kwa watu wengi kupanga safari na kushuhudia utafutaji wa mtandaoni wa vivutio vya kitalii vya nje ya nchi ukiongezeka, huku Thailand ikiwa maarufu zaidi.
Cheng Chaogong, mtafiti mkuu wa taasisi ya utafiti wa utalii inayohusishwa na wakala wa usafiri wa mtandaoni, Tongcheng-eLong, amesema kuwa nchi zilizo na sera rafiki kwa watu wa kutoka China kuingia kirahisi ndizo sehemu zinazopendelewa. Miongoni mwao, nchi za Kusini-Mashariki mwa Asia ziko juu ya orodha, pia kwa sababu ya hali ya hewa ya kupendeza inayopatikana katika majira ya wakati kama huu katika mwaka.
Bw. Nonglux Yooyendee, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Utalii ya Thailand katika Ofisi ya Shanghai alisema, watalii milioni 11 wa China walitembelea Thailand Mwaka 2019, ikiwakilisha robo ya idadi ya watalii wote wa kimataifa wanaoingia Thailand. Inakadiriwa kuwa watalii milioni 5 hadi 6 wa China watatembelea Thailand mwaka huu. Tangu Januari mwaka huu, Thailand imekaribisha watalii wapatao 90,000 kutoka China.
Kurejeshwa kwa utalii wa makundi na China, kunatazamwa kama nguvu mpya katika kufufuka kwa shughuli za utalii duniani kote, ambazo zimekuwa zikisuasua kutokana na janga la korona lakini pia kuwepo kwa mdororo wa kiuchumi.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma