Lugha Nyingine
Ripoti ya Umoja wa Mataifa yaonesha ongezeko la Uchumi wa Dunia unakadiriwa kufikia asilimia 1.9 Mwaka 2023
Picha hii iliyopigwa Septemba 14, 2020 ikionyesha mwonekano wa nje wa makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani. (Xinhua/Wang Ying)
UMOJA WA MATAIFA - Ripoti iliyotolewa na Umoja wa Mataifa Jumatano imesema, ongezeko la uzalishaji wa Dunia inakadiriwa kushuka hadi asilimia 1.9 Mwaka 2023 kutoka wastani wa asilimia 3.0 Mwaka 2022, ikiwa ni moja ya ongezeko la chini zaidi kuwahi kutokea katika miongo ya hivi karibuni.
Ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa ya Hali ya Kiuchumi na Matarajio ya Dunia Mwaka 2023 inakadiria ongezeko la uchumi wa dunia nzima litafikia asilimia 2.7 Mwaka 2024, huku baadhi ya changamoto za uchumi mkuu zikikadiriwa kuanza kupungua mwaka ujao.
Huku kukiwa na mfumuko mkubwa wa bei, ukazaji mkali wa sera za kifedha na kuongezeka kwa hali ya kutokuwa na uhakika, kushuka kwa sasa kwa uchumi kumepunguza kasi ya kufufuka kwa uchumi kutoka kwenye athari za UVIKO-19, na kutishia nchi kadhaa - zilizoendelea na zinazoendelea – huku kukiwa na makadirio ya kushuka kwa uchumi Mwaka 2023, ripoti hiyo imesema.
Ripoti imesema kasi ya ukuaji wa uchumi ilidhoofika kwa kiasi kikubwa nchini Marekani, Umoja wa Ulaya na nchi nyingine zilizoendelea Mwaka 2022, na kuathiri vibaya uchumi wa Dunia kupitia njia kadhaa.
Nchini Marekani, Pato la Taifa (GDP) linatarajiwa kupanuka kwa asilimia 0.4 pekee Mwaka 2023 baada ya makadirio ya ongezeko la asilimia 1.8 Mwaka 2022, ripoti hiyo imesema.
Mwanamke akipita karibu na supamaketi inayouza bidhaa kwa reja reja huko Arlington, Virginia, Marekani, Januari 18, 2023. (Xinhua/Liu Jie)
Ripoti hiyo imesema, ukuaji wa uchumi nchini China unatarajiwa kuimarika kwa wastani Mwaka 2023. Huku serikali ikirekebisha sera yake ya UVIKO-19 mwishoni mwa Mwaka 2022 na kurahisisha sera za bajeti na fedha, ukuaji wa uchumi wa China unakadiriwa kuongezeka hadi asilimia 4.8 Mwaka 2023.
Imeeleza kuwa kuimarika kwa hali ya kifedha duniani, pamoja na dola za Marekani zenye nguvu, kumezidisha udhaifu wa kifedha na madeni katika nchi zinazoendelea.
Nchi nyingi zinazoendelea zimeshuhudia ufufukaji wa polepole wa soko la ajira Mwaka 2022 na zinaendelea kukabiliwa na upungufu mkubwa wa ajira, ripoti imesema.
Ripoti hiyo inaonya kuwa ukuaji wa polepole wa uchumi, pamoja na mfumuko wa bei ulioinuliwa na udhaifu unaoongezeka wa madeni, unatishia kurudisha nyuma mafanikio yaliyopatikana kwa bidii katika maendeleo endelevu, na kuongeza athari mbaya za migogoro ya sasa.
Ripoti hiyo imezishauri serikali ziepuke hatua za kubana matumizi ya fedha ambazo zitazuia ukuaji wa uchumi na kuathiri vibaya makundi yaliyo hatarini zaidi, kuathiri maendeleo katika usawa wa kijinsia na matarajio ya maendeleo kwa vizazi vijavyo.
Wafanyakazi wakifanya kazi kwenye mstari wa kunda magari katika kituo cha Kaskazini cha Kampuni ya Magari ya Volkswagen- FAW cha China, katika Mji wa Tianjin, Kaskazni mwa China, Januari 11, 2023. (Xinhua/Zhao Zishuo)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma