Lugha Nyingine
China yarekodi ukuaji mdogo wa Fahirisi ya Bei ya Wanunuzi Mwaka 2022, yawa msaidizi wa kutuliza uchumi wa kimataifa
Wateja wakichagua bidhaa kwenye kituo cha maduka makubwa huko Shanghai, Mashariki mwa China, Oktoba 14, 2022. (Xinhua/Wang Xiang)
BEIJING - China imerekodi mfumuko mdogo wa bei Mwaka 2022, huku fahirisi ya bei za wanunuzi (CPI) ikiongezeka kwa asilimia 2 kutoka mwaka uliopita, ikiwa ni chini ya lengo la serikali la mwaka la asilimia 3.
Rekodi hiyo inatofautiana sana na kiwango cha juu cha mfumuko wa bei wa kimataifa na inathibitisha mchango wa China wa kusaidia uchumi wa Dunia uwe na hali tulivu katika wakati wa kukabiliana na shinikizo la kushuka kwa uchumi na kutokuwa na uhakika.
"Bei zimeendelea kuwa tulivu Mwaka 2022, jambo ambalo linadhihirisha kikamilifu uhimilivu wa uchumi wa China, ukubwa wa soko, na ufanisi wa hatua za kudumisha ugavi na utulivu wa bei," amesema Guo Liyan, mtafiti wa uchumi wa Akademia ya China ya Utafiti wa Uchumi Mkuu.
Fahirisi ya bei ya wazalishaji (PPI), ambayo hupima gharama za bidhaa kwenye lango la kiwanda, ilipanda kwa asilimia 4.1 katika kipindi cha Mwaka 2022. PPI ilipungua kwa asilimia 0.7 Mwezi Desemba, takwimu za Idara ya Taifa ya Takwimu ya China (NBS) zinaonyesha.
Tofauti kubwa na maeneo mengine duniani
Mfumuko mdogo wa bei wa China umekuwa wenye athari kidogo ikilinganishwa na nchi nyingine ambazo ziliathiriwa na kupanda kwa gharama za nishati na chakula, pamoja na kudorora kwa ugavi.
Mfumuko wa bei kwa mwaka mzima wa 2022 ulikuwa karibu asilimia 8 nchini Marekani, zaidi ya asilimia 8 katika ukanda unaotumia Fedha za Euro, na karibu asilimia 9 nchini Uingereza. Nchi zinazoibukia kiuchumi kama vile India, Brazili na Afrika Kusini zilishuhudia ukuaji wa bei wa asilimia 7 hadi 10 katika miezi 11 ya kwanza ya Mwaka 2022, amesema Wan Jinsong, ofisa wa Kamati Kuu ya Taifa ya Maendeleo na Mageuzi.
Mtazamo wa sasa
Kwa kutupia macho matarajio ya Mwaka 2023 -- ingawa bei za bidhaa za kimataifa zinaweza kubadilika kwa viwango vya juu na shinikizo la mfumuko wa bei kutoka nje bado lipo -- kuna msingi thabiti wa bei za wanunuzi bidhaa wa China kuendelea kuwa sawa, Wan amesema.
CPI inatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 2.1 katika kipindi cha Mwaka 2023, ikiwa ni juu kidogo kuliko ile ya Mwaka 2022, amesema Wen Bin, mchumi mkuu wa Benki ya Minsheng ya China.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma