Lugha Nyingine
Watengenezaji wa magari yanayotumia nishati mbadala wa China wagombea kutafuta sehemu kubwa ya soko
Watu wakitembelea Maonyesho ya 20 ya Kimataifa ya Magari ya Guangzhou katika Eneo la Uagizaji na Uuzaji Nje wa Bidhaa la China huko Guangzhou, Mkoa wa Guangdong, Kusini mwa China, Desemba 30, 2022. (Xinhua/Lu Hanxin)
GUANGZHOU - Katika Maonyesho ya 20 ya Kimataifa ya Magari ya Guangzhou yaliyomalizika hivi punde, watengenezaji wa magari wa China walionyesha maendeleo yao katika magari yanayotumia nishati mpya (NEV), wakionyesha nia na imani yao ya kugombea soko la magari yanayotumia nishati ya umeme na teknolojia za akili bandia.
GAC Aion, kampuni tanzu ya magari yanayotumia nishati mpya ya Kampuni ya Magari ya Guangzhou (GAC Group), ilizindua modeli yake mpya ya Hyper GT, iliyofuatiliwa na kutazamwa sana katika maonyesho hayo kutokana na muundo wake, udhibiti wake wa kuendeshwa kwa teknolojia za akili bandia na starehe ya muundo wake wa ndani.
Gu Huinan, meneja mkuu wa kampuni hiyo, amesema GAC Aion itazindua angalau modeli mbili mpya kila mwaka, na kuharakisha mkakati wake wa kujitokeza duniani ili kuwa chapa ya kiwango cha juu duniani katika soko la magari yenye kutumia teknolojia ya hali ya juu na akili bandia.
GAC Aion iliuza magari yanayokadiriwa kufika 271,000 katika Mwaka 2022, ikiwa ni ongezeko la asilimia 126 kutoka mwaka uliopita. Kwa mujibu wa Gu, chapa hiyo itajitahidi kuuza zaidi ya magari milioni 1.5 ifikapo Mwaka 2030.
Watengenezaji wakuu wa magari yanayotumia nishati mpya nchini China waliripoti ongezeko kubwa la mauzo Mwaka 2022 kutokana na upanuzi wa haraka wa soko na motisha za sera. Kampuni ya BYD, ambayo ni mtengenezaji mkuu wa magari yanayotumia nishati mpya wa China, imesema mauzo yake yaliongezeka kwa asilimia 208.64 mwaka hadi mwaka hadi kufikia zaidi ya magari milioni 1.86 katika Mwaka 2022.
Vyanzo mbalimbali vya habari ndani ya kampuni hiyo vimeliambia Shirika Habari la China, Xinhua kwenye maonyesho hayo kwamba, BYD imezindua teknolojia mfululizo, kama vile betri ya Blade, mifumo ya mseto ya DM-i na DM-p, e-Platform 3.0, na teknolojia ya ujumuishaji wa betri ya CTB, ili kukuza mageuzi ya tasnia ya kimataifa ya magari yanayotumia nishati mpya kufikia hatua kubwa ya maendeleo.
Takwimu zilizotolewa na Shirikisho la Watengenezaji Magari la China limeonesha kuwa, kuanzia Januari hadi Novemba 2022, mauzo ya magari yanayotumia nishati mpya nchini China yalizidi magari milioni 6.06, huku sehemu ya soko la magari hayo ikifikia asilimia 25.
Shirikisho hilo la watengenezaji magari linakadiri kuwa mauzo ya magari yanayotumia nishati mpya ya China kwa Mwaka 2023 yataongezeka kwa asilimia 35 mwaka hadi mwaka hadi kufikia magari milioni 9, ikilinganishwa na wastani wa magari milioni 6.7 kwa Mwaka 2022.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma