Lugha Nyingine
China yaweka mkazo katika kupata uhai wa kiuchumi baada ya kuondoa masharti ya kudhibiti UVIKO-19
Abiria wanaoingia nchini China wakiwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Pudong wa Shanghai, Mashariki mwa China, Januari 8, 2023. Kuanzia jana Jumapili, China ilianza kudhibiti UVIKO-19 kwa kutumia hatua za kupambana na magonjwa ya kuambukiza ya Ngazi ya B, badala ya magonjwa ya kuambukiza ya Ngazi ya A. (Xinhua/Ding Ting)
BEIJING - Karibu saa 12:30 asubuhi siku ya Jumapili, ndege ya NZ289 kutoka New Zealand ilitua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Pudong. Ilikuwa safari ya kwanza ya ndege ya kimataifa kuwasili Shanghai baada ya China kupunguza kwa kiasi kikubwa masharti yake ya kudhibiti UVIKO-19, ikimaanisha abiria wote waliokuwemo kwenye ndege hiyo hawatawekwa karantini kama ilivyokuwa siku za nyuma.
Shaly Rauss, abiria wa Ujerumani kwenye ndege hiyo anayeishi Shanghai, alikwenda New Zealand kwa ajili ya likizo wiki tatu zilizopita. "Najiona mwenye bahati sana. Tulikata tiketi mwaka mmoja uliopita. Sikujua wakati huo hili lingetokea. Tulikuwa tukitarajia kuwekwa karantini lakini sasa hatuhitaji kuwekewa karantini. Ninajisikia furaha sana," amesema baada ya kuwasili Shanghai.
China sasa inadhibiti UVIKO-19 kwa kufuata hatua dhidi ya magonjwa ya kuambukiza ya Ngazi ya B, badala ya magonjwa ya kuambukiza ya Ngazi ya A, katika mabadiliko makubwa ya sera yake ya kukabiliana na janga hilo.
Hatua hii ya kushusha udhibiti mkali wa UVIKO-19 itarahisisha usafiri wa raia wa China na nchi nyingine mbalimbali kwa njia rahisi na kwa utaratibu, kuongeza mabadilishano na ushirikiano wa kimataifa, na pia kusaidia kukuza uchumi wa Dunia.
Januari 9, Shirika la Ndege la Shandong litaanzisha usafiri wa ndege yake ya kwanza ya mkoa huo chini ya hatua mpya, kutoka Seoul, Korea Kusini hadi Jinan, Mkoa wa Shandong.
"Mabadiliko haya yanaleta urahisi kwa usafiri wa kuvuka mpaka. Sasa tunahimiza kikamilifu kurudisha na kufunguliwa kwa usafiri wa ndege kwenye njia za kimataifa na kikanda," amesema Wu Wanyuan, mkurugenzi wa kituo cha mawasiliano ya habari cha Shirika la Ndege la Shandong.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa hivi majuzi uliofanywa na Baraza la Kukuza Biashara ya Kimataifa la China, asilimia 91 ya mashirika ya biashara ya nje na mashirika ya biashara yaliyofanyiwa utafiti yanaunga mkono kikamilifu sera za China za kukabiliana na mlipuko wa Virusi vya Korona, huku asilimia 99.4 ya makampuni ya kigeni yaliyohojiwa yamesisitiza juu ya matarajio ya kukua kwa uchumi wa China Mwaka 2023.
"Maboresho ya China na uondoaji wa hatua za kuzuia janga na kuanza tena kwa utaratibu kwa usafiri wa ndege wa kimataifa kunatoa hali nzuri ya kufufua soko la kimataifa la usafiri wa ndege," amesema msemaji wa Shirikisho la Usafiri wa Ndege la China.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma