Lugha Nyingine
Idadi ya watalii wa kigeni nchini Tanzania yaongezeka kwa 64% ndani ya miezi 10
DAR ES SALAAM – Ofisa mmoja wa Tanzania jana Jumanne alisema idadi ya watalii wa kigeni waliotembelea nchi hiyo ya Afrika Mashariki kati ya Januari na Oktoba mwaka huu iliongezeka kwa asilimia 64.
Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi wa Idara ya Taifa ya Takwimu ya Tanzania, Daniel Masolwa, amesema watalii wa kigeni 1,175,697 walitembelea nchi hiyo kati ya Januari na Oktoba mwaka huu, ikilinganishwa na watalii 716,741 katika kipindi kama hicho Mwaka 2021.
"Idadi ya watalii imeongezeka kwa 458,956, ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 64," Masolwa amesema kwenye mkutano na wanahabari katika mji mkuu wa Dodoma.
Masolwa amesema kuongezeka kwa watalii wa kigeni kunatokana na juhudi za serikali zinazolenga kuendeleza shughuli za utalii baada ya kukumbwa na janga la UVIKO-19.
Ameongeza kuwa filamu ya Royal Tour, ambayo ilikuwa sehemu ya kampeni iliyoanzishwa na Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania Mwaka 2021 iliyolenga kuihimiza Tanzania iwe nchi inayowavutia zaidi watalii duniani, na filamu hiyo ilichangia kwa sehemu kubwa katika kukuza ujio wa watalii kutoka nje ya nchi.
Masolwa pia amesema watalii wengi waliotembelea Tanzania wanatoka Ufaransa, Uingereza, Ujerumani, Italia, Marekani, Uganda, Rwanda, Kenya, Burundi na Afrika Kusini.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma