Lugha Nyingine
Kampuni kubwa ya teknolojia ya China Huawei yatoa maarifa ya hali ya juu ya TEHAMA kwa wanafunzi wa vyuo vikuu nchini Ethiopia
ADDIS ABABA - Kampuni kubwa ya teknolojia ya China Huawei, kupitia Mpango wake wa Seeds for the Future, imetoa mafunzo ya hali ya juu na kubadilishana uzoefu kuhusu teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) kwa wanafunzi wa vyuo vikuu nchini Ethiopia.
Mpango huo wa uhamishaji uzoefu na maarifa uliodumu kwa wiki moja, umetoa mafunzo kwa wanafunzi 66 kutoka vyuo vikuu 12 vya Ethiopia. Hafla ya kuhitimu pia imefanyika mtandaoni Jumatatu mbele ya maafisa wa Wizara ya Elimu ya Ethiopia, Huawei imesema katika taarifa yake Jumanne.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wanafunzi hao wamejifunza kuhusu teknolojia ya kisasa na uvumbuzi kutoka kwa wahadhiri mashuhuri katika maeneo muhimu kama vile 5G, mitandao na wingu.
Mwaka 2008, Huawei ilizindua Mpango wa Seeds for the Future ili kusaidia ukuzaji wa talanta za kidijitali katika jamii duniani kote. Tangu Mwaka 2016, mpango huo umekuwa ukitekelezwa kila mwaka nchini Ethiopia, na wanafunzi zaidi ya 200 wameshiriki.
Chen Mingliang, Mkurugenzi Mtendaji wa Huawei Ethiopia ambaye alihutubia hafla ya kuhitimu, amesema fursa hiyo inasaidia kukuza vipaji vya vijana wa Ethiopia katika TEHAMA ili kusaidia mustakabali wa nchi hiyo.
Zelalem Assefa, Mkuu wa TEHAMA na elimu ya kidijitali katika Wizara ya Elimu ya Ethiopia, amesema Huawei na Wizara ya Elimu zimeshirikiana katika mpango huo kwa miaka mingi. Afisa huyo pia ametoa pongezi zake kwa wanafunzi walioshiriki katika programu hii na kuipongeza Huawei kwa kusaidia vipaji vya vijana.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma