Lugha Nyingine
Uchumi wa China wastawi kwa kufungua mlango kwa upana zaidi katika muongo mmoja uliopita
Picha hii iliyopigwa Tarehe 2 Novemba 2022 ikionyesha lango la Magharibi la Kituo cha Taifa cha Mikutano na Maonyesho cha Shanghai, ukumbi mkuu wa Maonesho ya Tano ya Kimataifa ya Uagizaji Bidhaa ya China (CIIE), huko Shanghai, Mashariki mwa China. (Xinhua/Fang Zhe)
BEIJING – Ili kuvuka mabadiliko ya mazingira ya kimataifa katika muongo mmoja uliopita, China imeendelea kuwa mtetezi thabiti wa uchumi ulio wazi wa Dunia, huku hatua madhubuti zikichukuliwa na maendeleo ya pande zote yamepatikana katika juhudi zake za kufungua mlango.
Katika Mkutano wa 29 wa Viongozi wa nchi zinazounda Ushirikiano Kiuchumi wa Asia na Pasifiki, China ilisisitiza nia yake ya kufungua mlango kwa kiwango cha juu, huku ikitoa wito kwa juhudi za kupanua ufunguaji mlango na kuboresha kikamilifu ushirikiano wa kiuchumi wa kikanda.
Juhudi thabiti za kufungua mlango, pamoja na ukuaji thabiti wa uchumi katika muongo mmoja uliopita, zimeifanya China kuwa eneo linalotafutwa sana na wawekezaji wa kimataifa.
Mwaka 2021, uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni katika China Bara, kwa matumizi halisi, ulizidi yuan trilioni 1 (kama dola za kimarekani bilioni 140.18) kwa mara ya kwanza, ikiwa ni asilimia 62.9 kuliko mwaka 2012 na kushika nafasi ya pili duniani.
Licha ya kudorora kwa uchumi wa Dunia mwaka huu, fedha za kigeni zinazoingia nchini humo ziliongezeka kwa asilimia 14.4 na kufikia karibu yuan trilioni 1.09 katika miezi 10 ya kwanza.
Bai Ming, mtafiti wa Taasisi Kuu ya Biashara ya Kimataifa na Ushirikiano wa Kiuchumi ya China chini ya Wizara ya Biashara ya China, anasisitiza ufanisi thabiti wa uchumi wa China, sera ya kufungua mlango isiyoyumba, mazingira bora ya biashara na ulinzi thabiti wa haki halali na maslahi ya wawekezaji wa kigeni kuwa sababu muhimu za kuvutia kwa uchumi wake.
Baada ya kuvuka kiwango cha Yuan trilioni 100 Mwaka 2020, Pato la Taifa la China (GDP) liliongezeka zaidi na kufikia zaidi ya yuan trilioni 114 mwaka jana, na kuchangia zaidi ya asilimia 30 katika ukuaji wa uchumi wa Dunia.
Mwaka 2012, Pato la Taifa la China lilifikia karibu yuan trilioni 53.86, ikiwa ni sawa na asilimia 11.5 ya jumla ya kimataifa.
Ukuaji huo thabiti umechochea upanuzi wa biashara. China sasa imekuwa mshirika mkuu wa kibiashara kwa zaidi ya nchi na kanda 140, huku biashara yake ya bidhaa na huduma ikifikia dola za kimarekani trilioni 6.9 Mwaka 2021 na kupata nafasi ya juu duniani kwa miaka miwili mfululizo.
Ikiwa na idadi ya jumla ya watu bilioni 1.4 na kundi la watu wa kipato cha kati ambao wanazidi milioni 400 na wanatarajiwa kupanuka zaidi, China inajivunia soko ambalo linatoa matumaini zaidi kwa uchumi wa Dunia.
Wakati ambapo uchumi wa Dunia unakabiliwa na kuongezeka kwa kujihami kiuchumi na changamoto nyingine kali, China, ikielekea kwenye maendeleo ya kisasa na nia thabiti ya kufungua mlango, imedhamiria kuunda fursa mpya kwa maendeleo ya kimataifa.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma