Lugha Nyingine
Ufufukaji wa uchumi wa viwanda wa China waonesha kuimarika licha ya faida kupungua
Mfanyakazi akifanya kazi kwenye kiwanda cha Harbin Electric Machinery cha Harbin Electric Corporation huko Harbin, Mkoa wa Heilongjiang, Kaskazini Mashariki mwa China, Septemba 3, 2022. (Xinhua/Wang Song)
BEIJING - Uchumi wa viwanda wa China unaonyesha dalili chanya zaidi za kuimarika licha ya kupungua kwa faida katika miezi tisa ya kwanza ya mwaka huu.
Makampuni makubwa ya viwanda, kila moja ikiwa na mapato ya kila mwaka ya biashara ya angalau yuan milioni 20 (dola milioni 2.79 za Kimarekani), yalishuhudia faida zao zikipungua kwa asilimia 2.3 katika miezi tisa ya kwanza hadi yuan trilioni 6.24, takwimu kutoka Idara ya Taifa ya Takwimu ya China (NBS) zimeonyesha Alhamisi.
Mwezi Septemba mwaka huu, kupungua kwa faida ya makampuni makubwa ya viwanda ilikuwa kwa asilimia 6 kutoka mwezi uliopita, takwimu zimeonyesha.
Mapato ya pamoja ya makampuni ya viwanda yalidumisha ukuaji wa haraka katika kipindi hicho, na kuongezeka kwa asilimia 8.2 na kufikia yuan trilioni 100.17.
Akiangazia uboreshaji wa muundo wa faida ya biashara, mtakwimu mkuu wa idara hiyo, Zhu Hong amesema kuwa ufanisi wa makampuni ya kiviwanda ulikuwa ukipata kasi ya kufufuka huku sera za kukuza uchumi zikianza kutekelezwa.
Jumla ya viwanda 19 kati ya 41 vikubwa vilishuhudia ukuaji wa faida katika kipindi cha Januari-Septemba. Sekta ya viwanda vya utengenezaji wa vifaa ilirejea katika ukuaji ikiwa na ongezeko la asilimia 0.6 , ikiongozwa na sekta ya mitambo ya umeme, ambayo ilishuhudia faida yake ikiongezeka kwa asilimia 25.3.
“Viwanda vya kutengeneza magari vilipata ukuaji wa faida wa asilimia 47.4 katika Mwezi Septemba, ukichochewa na urahisishaji wa minyororo ya viwanda na ugavi, na kuongezeka kwa uzalishaji wa magari yanayotumia nishati mpya,” Zhu amesema.
Zhu ameeleza kuwa, kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya umeme na ukuaji wa polepole wa bei ya makaa ya mawe, faida ya makampuni ya umeme ilipanda kwa asilimia 11.4 katika kipindi cha Januari-Septemba, na kuondoa kupungua kwa faida kulikodumu kwa zaidi ya mwaka mmoja.
Sekta ya madini iliendelea kushuhudia kuongezeka kwa faida, ikisukumwa na bei ya juu ya bidhaa, Zhu amesema.
Zhu pia amedokeza kuwa uendeshaji wa biashara za kibinafsi na ndogo uliendelea kuimarika, huku faida yao ikiongezeka kwa asilimia 1.5 katika kipindi hicho.
Takwimu hizo za Alhamisi pia zinaonyesha kuwa jumla ya mali ya makampuni ya viwanda ilifikia yuan trilioni 152.64 mwishoni mwa Septemba, ikiwa ni kuongezeka kwa asilimia 9.5 kuliko ile ya kipindi hicho cha mwaka uliopita.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma