Lugha Nyingine
Makala: Chinatown ya Botswana yaonyesha namna biashara kati ya China na Afrika inavyostawi
Watu wakionekana kwenye Mtaa wa Haskins wakiwa wamebeba bidhaa za China huko Francistown, Botswana, Julai 28, 2022. (Xinhua/Shingirai Madondo)
GABORONE, - Wakati Zhen Xiaojuan mwenye umri wa miaka 45 kutoka Mkoa wa Fujian, Mashariki mwa China alipoondoka nchini kwake na kuanzisha biashara yake nchini Botswana miaka 15 iliyopita, hakujua kwamba bidhaa zake zingeweza kuuzwa nje ya mipaka ya nchi hiyo ya Kusini mwa Afrika.
Mtaa wa Haskins huko Francistown, mji wa pili kwa ukubwa nchini Botswana, ambapo duka la Zhen linapatikana, sasa umekuwa mojawapo ya mitaa maarufu nchini humo.
Kuanzia alfajiri hadi jioni, maelfu ya bidhaa zinazotengenezwa nchini China zinazouzwa mitaani huvutia wananchi wengi na wanunuzi wa jumla kutoka Botswana na nchi jirani, hadi Zimbabwe, Zambia, Malawi na Lesotho. Kuanzia nguo, samani, vifaa vya matumizi ya nyumbani na baiskeli hadi vifaa vya kielektroniki kama vile televisheni, redio na simu za mkononi na pikipiki, bidhaa kutoka China zimewapa watu wa Botswana machaguo yenye nafuu na bora.
"Bidhaa zinazotengenezwa nchini China zimevutia Wabotswana, Wazimbabwe, Wazambia na Basotho (watu kutoka Lesotho). Na tunaanzisha Chinatown ndogo hapa Francistown," Zhen, ambaye anauza nguo, viatu, duveti, vidali na bidhaa za urembo ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua katika mahojiano.
Wafanyabiashara wachache wa China, hasa kutoka Mkoa wa Fujian, Mashariki mwa China, karibia Mwaka 2005 walianza biashara zao huko Francistown, umbali wa karibu kilomita 430 Kaskazini-Mashariki mwa Gaborone, mji mkuu wa Botswana. “Hata hivyo, katika miaka iliyofuata, jamii ya wafanyabiashara wa China imeanza kuongezeka taratibu,” anasema.
Weng Yongbiao, Mwenyekiti wa Shirikisho la Wafanyabiashara wa China la Francistown, anasema angalau wanachama 70 wamejiandikisha uanachama wao na shirikisho hilo.
"Lakini tunatarajia Wachina wengi zaidi kuja Francistown kufanya biashara. Hii inachochewa na uhusiano unaoendelea kushamiri kati ya China na Botswana," amesema Weng, huku akiongeza kuwa watu wa Botswana ni wakarimu sana na wamerahisisha wafanyabiashara wa China kuigeuza Botswana kuwa sehemu ya kusambaza bidhaa zinazotengenezwa nchini China kufikia nchi nyingine.
Wanunuzi wa jumla wakiwa kwenye duka lililojaa bidhaa za China katika Mtaa wa Haskins huko Francistown, Botswana, Julai 28, 2022. (Xinhua/Shingirai Madondo)
Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni zilizotolewa na Idara Kuu ya Forodha ya China, biashara kati ya China na Afrika mwaka jana ilifikia kiwango cha juu zaidi, ikionyesha ustahimilivu wakati wa janga la UVIKO-19.
Takwimu za hivi punde zinaonyesha kuwa jumla ya thamani ya biashara kati ya China na Botswana Mwaka 2021 ilifikia dola za Kimarekani milioni 428.1, ikiwa ni ongezeko la asilimia 32.6 mwaka hadi mwaka, huku Botswana ikiuza bidhaa zenye thamani ya dola milioni 172.6 nchini China, ikiwa ni ongezeko la asilimia 97.3 mwaka hadi mwaka.
Tafadzwa Mathambo, mhadhiri wa uchumi katika Chuo Kikuu cha Sheria na Mafunzo ya Kitaalamu cha Gaborone, anahusisha kupendwa kwa bidhaa za China na watu wa nchi nyingi jirani za Botswana na unafuu na ubora wake.
"Bidhaa za China zinakubaliwa kwa sababu zina bei nafuu na zina ubora mzuri," anasema Mathambo, huku akiongeza kuwa kutokana na kipato kupungua kwa baadhi ya watu na kudumaa kwa wengine, bidhaa za China zinatoa dili nzuri kwa wanunuzi na ajira kwa wauzaji.
Ellen Zimuto, mnunuzi wa bidhaa kutoka Zimbabwe, anasema, huwa anasafiri hadi Botswana mara mbili kwa mwezi kununua bidhaa kwa bei ya jumla kwa ajili ya kuziuza huko Bulawayo, mji wa pili kwa ukubwa nchini Zimbabwe, ambako ana duka. “Nimetengeneza fursa za ajira kwa watu watatu wanaofanya kazi kwenye duka langu wakati nikiwa safarini kununua bidhaa zaidi,” amesema Zimuto.
Kando na wale wanaofanya kazi katika maduka, baadhi ya wenyeji kama Tinny Mothobi wamepata sehemu kubwa ya kuuza chakula karibu na njia ya kwenda kwenye maduka yanayomilikiwa na Wachina. Amesema anatoa huduma za kifungua kinywa na chakula cha mchana kwa Wazimbabwe na Wazambia wanaokuja kununua bidhaa za China.
“Nawashukuru sana hawa Wachina kwani isingekuwa wao nisingeweza kuuza chakula kwa sababu idadi yetu ni ndogo,” amesema.
Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya Mwaka 2022, idadi ya watu nchini Botswana inakadiriwa kuwa 2,346,179.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma