Lugha Nyingine
Nchi za BRICS zaazimia kuimarisha ushirikiano wa kibiashara
Picha iliyopigwa Tarehe 17 Desemba, 2020 kutoka juu ikionyesha mandhari nzuri ya jengo la makao makuu ya Benki Mpya ya Maendeleo ya ushirikiano wa nchi za Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini (BRICS) katika Mji wa Shanghai, Mashariki mwa China. (Xinhua/Fang Zhe)
BEIJING - Wawakilishi wa biashara kutoka nchi za Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini (BRICS) jana Jumatano waliahidi kuimarisha ushirikiano wa kimataifa ili kulinda maslahi ya pamoja ya masoko yaliyoibuka na nchi zinazoendelea.
Wawakilishi hao wamekubaliana hayo kwenye Mkutano wa Mwaka 2022 wa Baraza la Biashara la BRICS uliofanyika Beijing, ambapo wawakilishi wapatao 150 kutoka vikundi kazi vya baraza hilo walihudhuria kupitia njia ya intaneti.
Taarifa ya pamoja kuhusu kujenga ushirikiano wa hali ya juu kati ya nchi za BRICS ilitolewa katika mkutano huo, ikitaka juhudi za kuhimiza mazungumzo na kuimarisha ushirikiano.
Mwenyekiti wa Baraza la Biashara la BRICS, Chen Siqing alisema China imeshirikiana na pande zote ili kutumia ipasavyo nguvu bora za kitaaluma na rasilimali na kukuza uchumi.
“China itashirikiana pamoja na jumuiya za wafanyabiashara kati ya nchi za BRICS na kushirikilia maendeleo yanayotokana na uvumbuzi ili kuongeza kasi ya ukuaji ya uchumi,” Chen aliongeza.
Baraza la Biashara la BRICS lilianzishwa wakati wa Mkutano wa tano wa BRICS uliofanyika Mwaka 2013 mjini Durban, Afrika Kusini, kwa lengo la kuhimiza na kuimarisha uhusiano wa kibiashara na uwekezaji miongoni mwa jumuiya za wafanyabiashara wa nchi tano za BRICS.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma