Lugha Nyingine
Benki ya Dunia yashusha makadirio ya kukua kwa uchumi wa Dunia Mwaka 2022 hadi asilimia 2.9
Picha iliyopigwa Arlington, Virginia, Marekani, Tarehe 7 Aprili 2021 ikionesha skrini inayomwonyesha Rais wa Benki ya Dunia David Malpass akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini Washington, D.C. Marekani wakati wa mikutano ya majira ya mchipuko ya Shirika la Fedha la Kimataifa na Benki ya Dunia. (Xinhua/Liu Jie)
WASHINGTON - Uchumi wa Dunia uko mbioni kukua kwa asilimia 2.9 katika Mwaka 2022, kiwango ambacho kimeshuka kwa asilimia 1.2 kutoka makadirio ya Januari mwaka huu, Benki ya Dunia imesema katika ripoti yake mpya ya Matarajio ya Uchumi wa Dunia iliyotolewa jana Jumanne, ikionya juu ya kudorora kwa kasi kwa uchumi.
Ripoti hiyo inasema, pamoja na uharibifu kutoka kwa janga la UVIKO-19, vita kati ya Russia na Ukraine vimechangia zaidi kushuka kwa uchumi wa Dunia, ambao unaingia katika kile ambacho kinaweza kuwa kipindi cha muda mrefu cha ukuaji duni na mfumuko wa bei ulio katika kiwango cha juu.
“Hii inaongeza hatari ya mdororo wa kiuchumi, na matokeo yanayoweza kudhuru uchumi wa nchi za kipato cha kati na cha chini” kwa mujibu wa ripoti hiyo.
Ripoti hiyo inaonesha kuwa, ukuaji wa uchumi wa Dunia unatarajiwa kushuka kutoka asilimia 5.7 Mwaka 2021 hadi asilimia 2.9 Mwaka 2022 na kubakia kwenye kiwango hicho cha ukuaji katika kipindi cha Mwaka 2023 hadi 2024.
Ukuaji wa uchumi katika nchi zenye uchumi mkubwa unatarajiwa kushuka kutoka asilimia 5.1 Mwaka 2021 hadi asilimia 2.6 Mwaka 2022.
Katika nchi zinazoibukia kiuchumi, ukuaji pia unatarajiwa kushuka kutoka asilimia 6.6 Mwaka 2021 hadi asilimia 3.4 Mwaka 2022, kiwango ambacho ni chini ya wastani wa asilimia 4.8 kwa mwaka kwa kipindi cha Mwaka 2011-2019.
Kutokana na madhara ya uharibifu yaliyosababishwa janga la UVIKO-19 na vita, kiwango cha pato la kila mtu katika nchi zinazoendelea mwaka huu kitakuwa karibu asilimia 5 chini ya mwelekeo wake wa kabla ya janga.
Rais wa Benki ya Dunia David Malpass amesema kuwa kwa nchi nyingi, mdororo wa uchumi utakuwa mgumu kuepukika, akiongeza kuwa ni muhimu kuhimiza uzalishaji na kuepuka vizuizi vya biashara.
"Mabadiliko katika sera za kibajeti, fedha, tabianchi na madeni yanahitajika ili kukabiliana na mgao usiyo sahihi na usiyo na usawa wa mitaji," Malpass amesema.
Ripoti hiyo inaonya kwamba, ikiwa mfumuko wa bei utaendelea kuwa juu, kurudiwa kwa hali ya kipindi cha awali cha mdororo wa uchumi kunaweza kutafsiriwa kuwa kushuka kwa kasi kwa uchumi wa Dunia pamoja na athari katika mifumo ya kifedha katika baadhi ya masoko yanayoibukia na nchi zinazoendelea.
"Nchi zinazoendelea zitalazimika kusawazisha hitaji la kuhakikisha uendelevu wa kifedha na hitaji la kupunguza athari za misukosuko ya sasa kwa raia maskini zaidi," Ayhan Kose, Mkurugenzi wa Kundi la Matarajio la Benki ya Dunia.
Mtembea kwa miguu akipita kwenye makao makuu ya Benki ya Dunia huko Washington, D.C., Marekani, Aprili 20, 2022. (Xinhua/Liu Jie)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma