Lugha Nyingine
Uchumi wa Tanzania Bara waongezeka kwa asilimia 4.9 Mwaka 2021
DAR ES SALAAM - Benki Kuu ya Tanzania Jumatatu wiki hii imeelezea ukuaji wa uchumi wa nchi hiyo uliorekodiwa Mwaka 2021 kuwa wenye kuridhisha.
Benki Kuu ya Tanzania imesema katika taarifa yake kwamba uchumi wa Tanzania Bara uliongezeka kwa asilimia 4.9 Mwaka 2021, ikiwa ni chini kidogo ya lengo la awali la kuongezeka kwa asilimia 5. Wakati huo huo, benki hiyo imeripoti kwamba uchumi wa Zanzibar uliongezeka kwa asilimia 5.1 Mwaka 2021, ikiwa pia ni kwa kiwango cha chini ikilinganishwa na lengo la asilimia 5.2.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uchumi wa Dunia uliendelea kukabiliwa na changamoto za kupanda kwa mfumuko wa bei, bei ya juu ya bidhaa, kuzuka upya kwa UVIKO-19, na usumbufu wa ugavi unaosababishwa na mgogoro kati ya Russia na Ukraine.
"Changamoto zimeongeza hatari katika kufufua shughuli za kiuchumi za kimataifa na ndani," imesema taarifa hiyo ambayo ilitolewa mwishoni mwa mkutano wa kamati ya sera za kifedha.
Taarifa hiyo imesema kwamba, mfumuko wa bei ulikuwa mkubwa Mwaka 2021/2022 kuliko mwaka uliopita, kutokana na kupanda kwa bei za bidhaa, hasa mafuta na bidhaa za walaji.
Imeongeza kuwa mzunguko wa pesa ulipanuka kulingana na lengo, ukiwa umeimarishwa na sera rafiki za kifedha na kuboreshwa kwa hali ya biashara.
Taarifa hiyo imesema kuwa ongezeko la mikopo ya sekta binafsi lilikuwa asilimia 13.4, ikiwa ni zaidi ya lengo la angalau asilimia 10.6; na uendeshaji wa kibajeti ulikuwa kwenye mwelekeo mzuri, huku ukusanyaji wa mapato ukifufuka vema, sambamba na shughuli za kiuchumi na kuboreshwa kwa ulipaji wa kodi.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma