Lugha Nyingine
Rais Xi atoa wito wa mataifa yote kuungana ili "kuvuka dhoruba, kusafiri kwa mustakabali mzuri"
BEIJING - Akizifananisha nchi zote duniani kama "abiria ndani ya meli moja ambao wana safari ya kufika pamoja," Rais Xi Jinping wa China siku ya Alhamisi wiki hii ametoa wito kwa "abiria wote" kuvuta kwa pamoja ili meli iweze kuvuka dhoruba na kuelekea kwenye mustakabali mzuri wa siku zijazo.
"Tukikabiliwa na changamoto nyingi, hatupaswi kupoteza kujiamini, kusitasita au kukurupuka. Badala yake, ni lazima tuimarishe imani na kusonga mbele na kukabiliana na matatizo yote," Xi amesema katika hotuba aliyoitoa kwa njia ya video kwenye ufunguzi wa Mkutano wa Mwaka 2022 wa Baraza la Asia la Boao.
Dunia bado haijatoka kwenye kivuli cha janga la mara moja katika karne, lakini hatari mpya za kiusalama tayari zinaibuka, Xi amesema, huku akisisitiza kwamba kaulimbiu ya mkutano wa mwaka huu ya "UVIKO-19 na Baada: Kufanya juhudi za pamoja kwa Maendeleo ya Dunia na mustakabali wa pamoja wa siku za baadaye" ni muhimu zaidi kwa hivi sasa.
Picha iliyopigwa Aprili 19, 2022 ikionyesha Kituo cha Mikutano ya Kimataifa cha Baraza la Asia la Boao (BFA) huko Boao, Mkoa wa Hainan wa China. (Xinhua/Yang Guanyu)
Usalama kwa Wote
Katika ufunguzi huo wa mkutano, Xi amependekeza Mpango wa Usalama wa Dunia ili kuhimiza usalama kwa watu wote duniani.
"Ni muhimu kwamba tuendelee kujitolea kwa maono ya usalama wa pamoja, wa kina, wa ushirikiano na endelevu, na kufanya kazi pamoja kudumisha amani na usalama duniani," amesema.
Ametoa wito wa kujitoa katika kuheshimu mamlaka ya nchi na ukamilifu wa eneo la nchi zote, kushikilia kutoingilia mambo ya ndani, na kuheshimu machaguo huru ya njia za maendeleo na mifumo ya kijamii yaliyofanywa na watu katika nchi tofauti.
Amesisitiza kuendelea kujitolea kufuata madhumuni na kanuni za Mkataba wa Umoja wa Mataifa, kukataa mawazo ya Vita Baridi, kupinga msimamo wa upande mmoja, na kusema hapana kwa siasa za makundi na mapambano ya kambi, ambayo yatazidisha changamoto za usalama katika Karne ya 21.
Rais Xi Jinping wa China akitoa hotuba kwa njia ya video kwenye ufunguzi wa Mkutano wa Mwaka wa Boao kwa ajili ya Bara la Asia 2022, Aprili 21, 2022. (Xinhua/Huang Jingwen)
“Wasiwasi halali wa kiusalama wa nchi zote unapaswa kuzingatiwa kwa uzito”, amesema Xi, akisisitiza umuhimu wa kupinga mikakati ya kiusalama ya nchi kwa gharama ya usalama wa nchi zingine.
Ametoa wito wa kuunga mkono juhudi zote zinazofaa kwa utatuzi wa amani wa migogoro, kukataa tabia za ndumila kuwili, na kupinga matumizi mabaya ya vikwazo vya upande mmoja na mamlaka ya mkono mrefu.
Familia ya Asia yenye Umoja na Maendeleo
"Tunahitaji kuendelea kuhimiza na kuimarisha Asia, kudhihirisha uthabiti, hekima na nguvu zake, na kuifanya Asia kuwa nguzo ya amani ya Dunia, nguvu ya ukuaji wa uchumi wa Dunia na mwelekeo mpya wa ushirikiano wa kimataifa," Xi amesema.
Ameeleza kuwa Dunia inanufaika wakati Asia inapofanya vizuri, Xi amesisitiza umuhimu wa kulinda kwa uthabiti amani barani Asia, kuendeleza kwa nguvu ushirikiano wa Asia, na kuhimiza kwa pamoja mshikamano wa Asia.
Xi ametoa wito kwa nchi za Asia kufuata kanuni za kuheshimiana, kuwa na usawa, kunufaishana na kuishi pamoja kwa amani, kufuata kanuni ya ujirani mwema na urafiki, na "kuhakikisha kwamba siku zote tunaweka mustakabali wetu mikononi mwetu."
Picha iliyopigwa Aprili 15, 2022 ikionyesha mwonekano wa Bandari ya Yangshan ya Shanghai, Mashariki mwa China. (Xinhua/Ding Ting)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma