Lugha Nyingine
Marais wa China na Armenia wapeana pongezi ya maadhimisho ya miaka 30 ya uhusiano wa kidiplomasia
BEIJING - Rais wa China Xi Jinping na mwenzake wa Armenia, Vahagn Khachaturyan, leo Jumatano wamepeana pongezi katika kuadhimisha miaka 30 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili.
Katika salamu zake za pongezi, Xi amesema, China na Armenia ni washirika wenzi na marafiki wa jadi, na tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati yao miaka 30 iliyopita, uhusiano huo umedumisha mwelekeo mzuri na tulivu wa maendeleo huku hali ya kuaminiana kisiasa ikiimarika, mafanikio makubwa yamepatikana katika nyanja mbalimbali, na mabadilishano ya kitamaduni na kati ya watu na watu yanazidi kuwa karibu.
Xi amesema, tangu kuzuka kwa janga la UVIKO-19, watu wa pande hizo mbili wamesaidiana na kuungana mkono katika mapambano dhidi ya janga hilo, na kuonyesha urafiki wao mkubwa.
Xi amesema anatilia maanani sana maendeleo ya uhusiano kati ya China na Armenia, na yuko tayari kushirikiana na Rais Khachaturyan kuchukua maadhimisho ya miaka 30 ya uhusiano wa kidiplomasia kama fursa ya kusukuma mbele mafanikio zaidi katika uhusiano wa nchi hizo mbili na ushirikiano kati ya pande zote ili kunufaisha nchi hizo mbili na watu wake.
Katika ujumbe wake, Rais Khachaturyan amesema tangu kuanzishwa kwa uhusiano wao wa kidiplomasia miaka 30 iliyopita, Armenia na China zimeshuhudia ushirikiano wao katika maeneo mbalimbali ukileta mafanikio makubwa, na Armenia inatilia maanani sana maendeleo na mafanikio ya China, pamoja na wajibu wake katika jukwaa la kimataifa.
Amesema angependa kufanya kazi na Xi ili kufikia maendeleo endelevu na thabiti katika uhusiano wa kirafiki na ushirikiano kati ya Armenia na China kwa manufaa ya watu wa nchi hizo mbili.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma