Lugha Nyingine
Xi Jinping apongeza kuzinduliwa kwa Shule ya Uongozi ya Julius Nyerere
BEIJING - Xi Jinping, Katibu Mkuu wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), Jumatano wiki hii ametuma barua ya pongezi kwa uzinduzi wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere nchini Tanzania.
Shule hiyo ilianzishwa kwa pamoja na vyama sita vya ukombozi vya Kusini mwa Afrika: Chama Cha Mapinduzi cha Tanzania (CCM), Chama cha African National Congress cha Afrika Kusini (ANC), Chama cha Ukombozi cha Msumbiji (FRELIMO), Chama cha Harakati ya Ukombozi wa Watu cha Angola (MPLA), Chama cha SWAPO cha Namibia na Chama cha ZANU-PF cha Zimbabwe .
Akibainisha kuwa vyama hivyo sita vimeungana na kuwaongoza wananchi wao katika kujipatia uhuru na maendeleo ya nchi zao, Xi amesema uzinduzi wa Shule ya Uongozi ya Julius Nyerere utatoa jukwaa muhimu kwa vyama hivyo sita ili kuongeza uwezo wao wa utawala na kuongoza vyema nchi zao kwa ajili ya kupata maendeleo na kuwanufaisha watu wao.
Xi amesisitiza kwamba, wakati Dunia inakabiliwa na mabadiliko ambayo hayajatokea katika karne moja iliyopita, China na Afrika zinahitaji kuimarisha mshikamano na ushirikiano zaidi kuliko wakati mwingine wowote ili kukabiliana na hatari na changamoto, kuhimiza maendeleo ya pamoja na kuboresha ustawi wa watu.
Amesema, CPC kiko tayari kuchukua uzinduzi wa shule hiyo kama fursa ya kuimarisha mabadilishano ya uzoefu wa utawala wa serikali na vyama barani Afrika, kusaidiana katika kutafuta njia za maendeleo zinazoendana na hali halisi za nchi zao, kuimarisha ushirikiano halisi katika nyanja zote, kuhimiza ujenzi wa jumuiya yenye mustakabali wa pamoja kati ya China na Afrika kwa kiwango cha juu, na kuchangia zaidi katika ujenzi wa Dunia iliyo bora.
Kwa mujibu wa Gazeti la Serikali ya Tanzania, Daily News Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan aliwaongoza mamia ya wananchi na viongozi wawakilishi wa nchi hizo sita za Ukanda wa Kusini mwa Afrika katika uzinduzi wa shule hiyo.
Gazeti hilo limeripoti kwamba, ujenzi wa shule hiyo umefadhiliwa na Serikali ya China chini ya ushirikiano wa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) na vyama hivyo vya ukomboni vya Kusini mwa Afrika na umegharimu takribani dola za kimarekani milioni 45.
“Hii siyo kusherehekea jengo ambalo limejengwa bali pia historia ambayo inatengeneza mrengo wa uhuru kama ulivyopiganiwa na viongozi na waasisi wetu kama Mwalimu Nyerere” amesema Afisa wa chama cha ANC katika mahojiano na Daily News ambaye alimwakilisha Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa kwenye uzinduzi wa shule hiyo iliyojengwa eneo la Kibaha, Mkoa wa Pwani, Mashariki mwa Tanzania
Julius Nyerere alikuwa ni Rais wa kwanza wa Tanzania ambaye aliisaidia Tanzania na nchi za Kusini mwa Afrika kujipatia uhuru kutoka kwa wakoloni. Kutokana na Mchango wake barani Afrika, na kwenye uhusiano wa China na Afrika nchi hizo ziliamua kujenga shule hiyo na kuipa jina la Julius Nyerere.
Mwaka 2018 aliyekuwa Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa shule hiyo ambao sasa umekamilika.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma